Lugha Nyingine
Rais wa Iran aagiza kuanza kwa mazungumzo na Marekani kuhusu suala la nyuklia

Picha hii iliyopigwa Februari 1, 2026 ikionyesha mandhari ya mji wa Tehran, Iran. (Xinhua/Shadati)
TEHRAN - Rais wa Iran Masoud Pezeshkian ameagiza kuanza kwa mazungumzo na Marekani katika mfumo wa suala la nyuklia, shirika la habari la Fars limeripoti jana Jumatatu, likinukuu chanzo cha serikali kisichotajwa jina.
Shirika hilo, limenukuu kauli za msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran Esmaeil Baghaei mapema siku hiyo akisema kuwa mazungumzo hayo kati ya Iran na Marekani huenda yatafanyika nchini Uturuki katika siku chache zijazo.
Wakati huo huo, shirika la habari la Tasnim likinukuu chanzo cha habari kisichotajwa jina, pia limethibitisha kwamba maafisa waandamizi kutoka pande hizo mbili huenda wataanza mazungumzo katika siku zijazo.
Mazungumzo hayo huenda yakafanyika kati ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi na Mjumbe Maalum wa Rais Donald Trump wa Marekani Steve Witkoff, shirika la Tasnim limeripoti, likiongeza kuwa mahali na tarehe halisi ya mazungumzo hayo bado hayajaamuliwa.
Hatua hizo mpya zinakuja huku mvutano kati ya Tehran na Washington ukiendelea kuwa mkubwa, wakati shughuli za kijeshi za Marekani zikiongezeka Mashariki ya Kati. Utawala wa Trump ulituma kundi la manowari za kubeba ndege za kivita na meli kadhaa za kivita katika eneo hilo la Mashariki ya Kati mwishoni mwa Januari.
Siku ya Jumapili, Trump alisema kuwa iwapo Tehran itashindwa kufikia makubaliano ya nyuklia na Washington, "tutagundua" kama Kiongozi Mkuu wa Iran Ali Khamenei alikuwa sahihi kuonya kwamba shambulizi la Marekani linaweza kuzua vita vya kikanda.
Wakati huo huo, Araghchi alisema Jumapili kwenye mahojiano na CNN kwamba makubaliano ya nyuklia "yenye haki, ya usawa, na ya ulinganifu" kati ya Iran na Marekani bado yanaweza kufikiwa katika muda mfupi, mradi Washington itaachane na sera yake ya kulazimisha.
Mapema jana Jumatatu, Baghaei aliuambia mkutano na waandishi wa habari wa kila wiki mjini Tehran kwamba Iran inapitia maelezo na muhtasari wa jumla kuhusu uwezekano wa kuanzisha mazungumzo na Marekani.

Picha hii iliyopigwa Februari 1, 2026 ikionyesha mandhari ya mji wa Tehran, Iran. (Xinhua/Shadati)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



