China yazindua kampeni ya manunuzi ili kuongeza matumizi wakati wa likizo ya Mwaka Mpya wa Jadi

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Februari 03, 2026

Watu wakinunua mapambo ya sikukuu kwenye jengo la maduka mengi katika Mji wa Beijing, China, Januari 31, 2026. (Xinhua/Li Xin)

Watu wakinunua mapambo ya sikukuu kwenye jengo la maduka katika Mji wa Beijing, China, Januari 31, 2026. (Xinhua/Li Xin)

BEIJING - China itazindua kampeni maalum ya manunuzi ya siku tisa wakati wa likizo ya Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi ili kuongeza matumizi, kuboresha maisha ya kitamaduni, na kuchochea nguvu hai za soko, Wizara ya Biashara ya China (MOC) imetangaza jana Jumatatu.

Kampeni hiyo, iliyopangwa kuanza Februari 15 hadi Februari 23, inashirikisha shughuli katika maeneo sita, ikiwa ni pamoja na migahawa, malazi, usafiri, utalii, manunuzi na burudani, kwa mujibu wa mpango kazi uliotolewa kwa pamoja na MOC na idara zingine nane za serikali.

Hatua hizo zikiwemo za kuhimiza kula vyakula migahawani na karamu za mijumuiko ya watu wakati wa sikukuu, kutoa punguzo la bei kwa vifaa vya matumizi ya nyumbani vinavyotumia umeme na ukarabati wa nyumba, kuongeza uwezo wa usafiri, kuandaa matukio ya matumizi ya kitamaduni na utalii katika nchi nzima, na kuanzisha promosheni za manunuzi katika maeneo makuu ya kibiashara na punguzo la bei za tiketi za sinema.

Msisitizo mkubwa pia umewekwa kwenye upanuzi wa mipango ya kutoa ruzuku kwa watu kununua vitu vipya kwa kubadilishana na vya zamani, huku ruzuku ikiongezwa kwa bidhaa za matumizi ili kuunga mkono maduka halisi ya ana kwa ana ya rejareja.

Aidha, serikali inakusudia kurahisisha mazingira ya malipo kwa wasafiri wa kimataifa kwa kuboresha kadi za benki, malipo ya kutumia simu, na huduma za pesa taslimu, ili kuhakikisha matumizi yasiyotatizwa kwa watalii wanaoingia China.

Sikukuu ya Mwaka Mpya wa Jadi wa China, ambayo ni likizo muhimu zaidi ya jadi nchini China, kwa kawaida huwa ni msimu wa kilele kwa matumizi ya wanunuzi, unaochochewa na mijumuiko ya familia, usafiri, milo, burudani na ununuzi wa zawadi.

Kwa kuwa mahitaji ya ndani yanaendelea kuwa kichocheo muhimu cha ukuaji wa uchumi, mamlaka za China zimeanzisha mfululizo wa hatua za sera zinazolenga kufungua zaidi uwezo wa matumizi na kutuliza matarajio ya soko wakati wa kipindi hicho cha likizo.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha