Lugha Nyingine
Trump asema "hakuna tarehe ya mwisho" ya kufikiwa makubaliano ya amani ya Ukraine

Picha iliyopigwa kutoka kwenye video iliyotolewa na Ikulu ya Marekani White House ikimwonesha Rais wa Marekani Donald Trump akikutana na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky kwenye eneo la Mar-a-Lago huko Palm Beach, Florida, Marekani, Desemba 28, 2025. (Xinhua)
WASHINGTON - Rais Donald Trump wa Marekani amesema hana hakika kama makubaliano ya amani kuhusu mgogoro wa Ukraine yataweza kufikiwa kabla ya mwisho wa mwaka 2025.
"Sina tarehe ya mwisho. Unajua tarehe yangu ya mwisho ni ipi? Ni kumaliza vita," Trump amewaambia waandishi wa habari jana Jumapili wakati wa kuanza kwa mkutano wake na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky aliyemtembelea katika eneo lake la Mar-a-Lago huko Palm Beach, Florida.
Alipoulizwa kama mazungumzo yao hayo ya Jumapili yatafikia makubaliano ya amani, Trump alisema: "Inategemea -- naamini tuna njia za kufikia makubaliano," akisema kuwa mgogoro huo wa Ukraine umethibitika kuwa mgumu kuutatua.
Kwa upande wake Rais Zelensky amesema mazungumzo yake na Trump yatajikita katika rasimu mpya ya mpango wa amani wenye vipengele 20 na mpangilio wa utatuzi.
"Ni muhimu sana timu zetu kujadili mkakati – namna ya kufanya hatua kwa hatua, na kuleta amani karibu zaidi," Zelensky amesema.
Kabla ya mkutano huo na Zelensky, Trump aliandika kwenye Mtandao wa Truth Social akisema kwamba "alikuwa na mazungumzo mazuri na yenye tija sana" na Rais wa Russia Vladimir Putin.
Kwenye mazungumzo hayo ya simu, Trump na Putin walikubaliana kwamba usimamishaji mapigano kwa muda utaongeza tu muda wa mgogoro huo wa Ukraine, Msaidizi wa Rais wa Russia Yuri Ushakov amesema.
Marais hao wawili "wana maoni sawa kwa upana kwamba usimamishaji mapigano wa muda uliopendekezwa na Ukraine na Ulaya, kwa kisingizio cha kujiandaa kwa kura ya maoni au visingizio vingine, utaongeza tu muda wa mgogoro huo na hatari ya kurejea kwa uhasama," Ushakov amesema.
Kwenye mazungumzo hayo ya Florida, Trump na Zelensky wanatarajiwa kujadili mipango ya kusimamisha mapigano, pendekezo la kuanzisha eneo maalum lisilo na shughuli za kijeshi, usimamizi wa mtambo wa nyuklia wa Zaporizhzhia, udhibiti wa ardhi ya eneo la Donbas, na mahakikisho ya usalama baada ya kuisha kwa mgogoro huo.

Picha hii ya kumbukumbu ikionyesha eneo la Mar-a-Lago huko Palm Beach, Florida, Marekani. (Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



