Lugha Nyingine
China Kusukuma Maboresho ya Elimu ya Juu Katika Miaka 5 Ijayo

Mhitimu akiweka kofia ya joho kwa ajili ya mwanafunzi mwenzake kabla ya sherehe ya kuhitimu katika Chuo Kikuu cha Peking mjini Beijing, mji mkuu wa China, Julai 2, 2025. (Xinhua/Chen Shuo)
BEIJING - China itapanua na kuboresha elimu ya juu, kwa kuongeza udahili katika programu bora za shahada ya kwanza, kwa mujibu wa mapendekezo kuhusu mpango utakaoongoza maendeleo ya nchi hiyo katika miaka mitano ijayo.
Hilo limeelezwa kwenye mapendekezo ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) kwa ajili ya kuandaa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa nchi hiyo (2026-2030) kwa maendeleo ya uchumi na kijamii, ambayo yalipitishwa katika mkutano muhimu wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama hicho wiki iliyopita na kutangazwa kwa umma juzi Jumanne.
Wakati wa kipindi cha Mpango wa 14 wa Miaka Mitano, kiwango cha jumla cha udahili wa wanafunzi katika elimu ya juu nchini China kilifikia asilimia 60.8, huku wanafunzi milioni 55 wakihitimu kutoka vyuo vikuu.
Zhang Nanxing, mkurugenzi wa taasisi ya elimu ya juu katika Akademia ya Taifa ya Sayansi za Elimu ya China, amesema kuwa mipangilio na mahitaji mapya yamefafanua zaidi mwelekeo wa kimkakati kwa ajili ya mageuzi ya elimu ya juu na kuwaandaa watu wenye ujuzi.
Zeng Tianshan, naibu mkurugenzi wa taasisi ya mtaala na vitabu vya kiada chini ya Wizara ya Elimu ya China, amesema mapendekezo hayo yatasaidia kupanua rasilimali za elimu zenye ubora wa juu kwa makundi zaidi, hivyo kuboresha usawa na ubora wa elimu, na kuingiza msukumo mpya katika kuwaandaa watu wenye ujuzi wa uvumbuzi.
"Wakati wa kutekeleza mapendekezo hayo, vyuo vikuu vinapaswa kuandaa kozi na mipangilio ya programu zinazoendana na mikakati ya kitaifa, na kuzifanya zihusiane zaidi na kuendana zaidi na kuwaandaa watu wenye ujuzi, ili kuimarisha vyema kazi ya elimu katika kuhudumia maendeleo ya kiuchumi na kijamii," Zeng ameongeza.
Mbali na elimu ya juu, mapendekezo hayo yanatoa wito wa kupanua kwa kasi tulivu utoaji wa elimu ya bure na kuchunguza upanuzi wa urefu wa wa muda wa elimu ya lazima.
Mfumo wa sasa wa elimu ya lazima wa China unachukua muda wa miaka tisa, kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya sekondari ya chini. Mwaka 2024, wanafunzi zaidi ya milioni 34.6 wapya walidahiliwa katika elimu ya lazima kote nchini China, ikifanya jumla ya wanafunzi katika hatua hiyo kufikia milioni 159.7.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



