Lugha Nyingine
Marais wa China na Marekani wakutana huko Busan, Korea Kusini

(Picha/Xinhua)
Rais Xi Jinping wa China na mwenzake wa Marekani Donald Trump wamekutana na kufanya mazungumzo huko Busan, Korea Kusini leo Alhamisi.
Kwenye mazungumzo hayo, Rais Xi amesema, tangu Rais Trump aingie madarakani, wameshafanya mazungumzo mara tatu kwa njia ya simu na kutumiana barua kadhaa, huku wakidumisha mawasiliano ya karibu.
Amesema chini ya mwongozo wa pamoja, uhusiano kati ya nchi hizo mbili umeendelea kuwa tulivu kwa ujumla.
Amesema, siku kadhaa zilizopita, wajumbe wa biashara na uchumi wa nchi hizo mbili walifanya duru mpya ya mazungumzo huko Kuala Lumpur, wakifikia makubaliano ya kimsingi juu ya kutatua masuala makuu yanayofuatiliwa na kila upande, ambayo yameweka mazingira wezeshi kwa mkutano huo wa leo kati ya marais hao.
Rais Xi amesema, kutokana na hali tofauti kati ya China na Marekani, baadhi ya tofauti haziwezi kuepukika. Ameeleza kuwa, zikiwa ni nchi mbili zenye uchumi mkubwa zaidi duniani, kuwa na mikwaruzano ni jambo la kawaida.
Amesema yeye na Rais Trump wakiwa wakuu wa nchi, wanapaswa kuelekeza vizuri mwelekeo, kudhibiti vyema hali ya jumla na kuhakikisha meli kubwa ya uhusiano kati ya China na Marekani inasonga mbele kwa utulivu.
Rais Xi amesisitiza kuwa maendeleo na ustawi wa China vinakwenda bega kwa bega na dhamira ya Rais Trump ya“Make America Great Again”na kwamba nchi hizo mbili zinaweza kusaidiana kufanikiwa na kustawi pamoja.
"China na Marekani zinapaswa kuwa washirika na marafiki. Hivyo ndivyo historia imetufundisha na ndivyo uhalisia unahitaji" amesema Rais Xi.
Pia amesema kuwa anapenda kuendelea kushirikiana na Rais Trump kujenga msingi imara kwa uhusiano kati ya China na Marekani na kuweka mazingira mazuri kwa maendeleo ya nchi zote mbili.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



