Lugha Nyingine
Maonyesho yafunguliwa nchini Kenya ili kuongeza ushirikiano wa kilimo kati ya China na Afrika

Picha hii iliyopigwa Oktoba 28, 2025 ikionyesha hafla ya kufunguliwa kwa Maonyesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Afrika 2025 jijini Nairobi, Kenya. (Xinhua/Li Yahui)
NAIROBI - Maonyesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Afrika 2025 yamefunguliwa rasmi jana Jumanne katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, chini ya kaulimbiu ya "Kuongeza Nguvu ya Uzalishaji barani Afrika kupitia Uvumbuzi na Ufikiaji wa Soko" ili kuongeza ushirikiano kati ya China na Afrika katika kilimo cha kisasa.
Paul Kipronoh Ronoh, katibu mkuu katika Wizara ya Kilimo ya Kenya, amesema kwamba maonyesho hayo yanatafuta kuiweka Afrika katika nafasi ya kuwa kituo cha uvumbuzi wa kilimo na biashara duniani.
Amesema, maonyesho hayo yameshirikisha kampuni zaidi ya 150 kuonyesha bidhaa, zikiwemo kampuni 100 kutoka China, hii ni ishara kuwa nafasi ya Kenya ya kuwa kituo cha kikanda cha biashara ya kilimo na uvumbuzi inainuliwa siku hadi siku.
"Maonyesho haya yakiwa jukwaa la bara zima la Afrika, linalenga kuhimiza uvumbuzi, utumiaji wa teknolojia, na ufikiaji wa soko, ambavyo vyote ni nguvu muhimu ya kuhimiza mambo ya kilimo yabadilishe muundo wake." Ronoh amesema.
Amesema kuwa maonyesho hayo yanaimarisha dhamira ya Kenya kwa ushirikiano wa kilimo wa kikanda na wa kimataifa, hasa chini ya Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika na Mpango Jumuishi wa Maendeleo ya Kilimo barani Afrika wa Umoja wa Afrika.
Balozi wa China nchini Kenya Guo Haiyan amesema kampuni zaidi ya 100 za kilimo za China, zinazojikita katika kazi za kuandaa mbegu za mazao ya kilimo na utengenezaji wa vyakula vya mazao ya kilimo zinashiriki kwenye maonyesho hayo.
"Uvumbuzi huu unaweza kusaidia wakulima wa familia mojamoja kuongeza uzalishaji wa kilimo, kupunguza hasara baada ya mavuno, na kukifanya kilimo kuwa na uwezo wa kukabiliana na mishtuko ya tabianchi." Guo amesema, akiongeza kuwa kampuni hizo za China si kama tu zinaonyesha bidhaa bali pia zinatafuta ushirikiano, fursa za uwekezaji, ili kupata maendeleo kwa pamoja na wakulima na kampuni za Afrika.
Tito Mutai, afisa mtendaji mkuu wa Maonyesho hayo ya Kilimo ya Afrika amesema, wakati wa maonyesho hayo, makubaliano matano yatasainiwa kati ya China na Kenya ili kuongeza uwekezaji na biashara katika sekta ya kilimo kati ya nchi hizo mbili.
Mutai amesema, nchi zote mbili zitanufaika na matarajio ya pamoja ya kukibadilisha kilimo kuwa chanzo cha chakula vilevile kichocheo cha ukuaji wa jumuishi na kuongeza nafasi za ajira.

Mwonyeshaji bidhaa (kushoto) akielezea bidhaa kwa wageni kwenye Maonyesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Afrika 2025 jijini Nairobi, Kenya, Oktoba 28, 2025. (Xinhua/Li Yahui)

Guo Haiyan, Balozi wa China nchini Kenya, akitoa hotuba kwenye hafla ya kufunguliwa kwa Maonyesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Afrika 2025 jijini Nairobi, Kenya, Oktoba 28, 2025. (Xinhua/Li Yahui)

Paul Kipronoh Ronoh, katibu mkuu katika Wizara ya Kilimo ya Kenya, akitoa hotuba kwenye hafla ya kufunguliwa kwa Maonyesho ya Kilimo ya Kimataifa ya Afrika 2025 jijini Nairobi, Kenya, Oktoba 28, 2025. (Xinhua/Li Yahui)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



