Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia azishutumu Nchi za Magharibi kujiandaa kwa mgogoro mpya barani Ulaya

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 29, 2025

MINSK - Waziri wa Mambo ya Nje wa Russia Sergei Lavrov jana Jumanne wakati akitoa hotuba yake kwenye Mkutano wa 3 wa Kimataifa wa Minsk juu ya Usalama wa Eurasia ameonya kwamba nchi za Magharibi zinajiandaa waziwazi kwa mgogoro mkubwa barani Ulaya.

Lavrov amezilaumu nchi za Magharibi kwa kudhoofisha makubaliano ya udhibiti wa silaha na kuendelea na upanuzi wa Jumuiya ya Kujihami ya Nchi za Magharibi (NATO) kuelekea mashariki licha ya ahadi za awali za kufanya kinyume chake.

Lavrov amesema mgogoro nchini Ukraine umeharibu usanifu wa usalama wa Ulaya na Bahari ya Atlantiki, ukiugeuza Umoja wa Ulaya kuwa upanuzi wa NATO.

Amekosoa mapendekezo ya mfumo mpya wa usalama wa Ulaya ambao kimakusudi unazitenga Russia na Belarus, akirejelea Jumuiya ya Kisiasa ya Ulaya ya Ufaransa kuwa ni mfano wa mbinu za kutenga.

Akirejelea kupamba moto kwa shughuli za kijeshi, Lavrov ameutaja uratibu wa nyuklia kati ya Ufaransa na Uingereza, vilevile makubaliano ya kijeshi kati ya Ujerumani na Uingereza ambayo yanaweza kujumuisha vipengele vya nyuklia, kuongezeka kwa matumizi ya ulinzi, na mazoezi makubwa ya kijeshi kwa ajili ya kupelekwa mashariki.

Pia ameelezea wasiwasi wake juu ya kuongezeka kwa shughuli za NATO katika Bahari ya Aktiki, ambazo amesema zinatishia ushirikiano wa amani katika eneo hilo.

Waziri huyo amezishutumu nchi wanachama wa NATO za Ulaya kwa kuongeza muda wa mgogoro wa Ukraine kwa kusambaza silaha na kuishinikiza Marekani dhidi ya suluhu ya mazungumzo.

Ameelezea matumaini yake kwamba Rais wa Marekani Donald Trump ataendelea kuwa na dhamira ya kutatua mgogoro huo kwa msingi wa kanuni kutoka kwenye mkutano wa viongozi wa Alaska.

Lavrov amerudia tena wito wa Russia kwa mfumokazi jumuishi wa usalama ulioundwa ili kuzuia nguvu kutoka nchi yeyote kubwa na kuhimiza mfumo wa kweli wa ncha nyingi.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha