

Lugha Nyingine
Msako wa Marekani kwenye kiwanda cha betri wazua wasiwasi juu ya uwekezaji wa kigeni
Rais Donald Trump wa Marekani (kulia) akimkaribisha Rais Lee Jae-myung wa Korea Kusini (katikati) kwenye Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Agosti 25, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)
WASHINGTON - Mamlaka ya uhamiaji ya Marekani iliwashikilia wafanyakazi zaidi ya 300 wa Korea Kusini katika kiwanda cha kutengeneza betri huko Georgia wiki iliyopita wakati wa uchunguzi wa uhalifu kuhusu ukiukaji wa visa, ikizua hisia kali kutoka Korea Kusini na kuzua wasiwasi kuhusu uwekezaji wa kigeni wa siku za usoni nchini Marekani.
Rais Lee Jae-myung wa Korea Kusini, ambaye alikuwa punde tu amefanya ziara Marekani na kufanya mazungumzo na Rais Donald Trump wa Marekani mwishoni mwa mwezi Agosti, amelielezea tukio hilo kuwa ni "ukiukaji usio wa haki" na kusema kwamba anajihisi "kuwa na wajibu kubwa" kwa ajili ya kulinda raia wa Korea Kusini.
Katika kuitikia hali hiyo, Seoul ilimtuma Waziri wa Mambo ya Nje Cho Hyun kwenda Washington. Siku ya Jumatano, Cho alikutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio kujadili wafanyakazi hao waliozuiliwa na kuzitaka mamlaka za Marekani kuhakikisha kurejea kwao haraka bila kutatiza kurejea tena siku zijazo.
Ndege ya kukodi ya Shirika la Ndege la Korea iliyopangwa kuwarudisha nyumbani wafanyakazi hao waliozuiliwa iliwasili katika uwanja wa ndege wa Atlanta juzi Jumatano ambapo kwa mujibu wa shirika la habari la Korea Kusini Yonhap, ndege hiyo ilikuwa ikitarajiwa kuondoka jana Alhamisi ikiwa na raia hao 316 wa Korea Kusini.
Maafisa wa Marekani wametetea operesheni hiyo, wakiielezea lengo lake kuwa ni kutekeleza sheria za uhamiaji. Wamesema kuwa wengi wa watu hao waliozuiliwa waliingia Marekani kwa viza ya B-1 au ESTA, ambayo hairuhusu ajira. Bila kutoa maoni yoyote juu ya operesheni ya Georgia, msimamizi wa mambo ya mipaka wa White House Tom Homan ameapa kufanya operesheni zaidi katika maeneo ya kazini.
Hyundai na LG Energy Solution, wamiliki wa eneo lililolengwa, wamefafanua kuwa wafanyakazi waliozuiliwa walikuwa mafundi waliopewa mikataba midogo kwenye kazi za muda. Katika taarifa yake kuhusu msako huo, Hyundai imeahidi kufuata kikamilifu sheria na kanuni za uhamiaji za Marekani.
Akiwarejelea watu hao waliozuiliwa kuwa "wageni haramu" katika mahojiano, Trump amesisitiza kwenye mitandao ya kijamii kwamba Marekani inabaki kuwa wazi kwa uwekezaji wa kigeni, mradi tu kampuni zitatii kanuni za uhamiaji za Marekani.
Hata hivyo, alipokuwa akielezea kucheleweshwa kwa siku moja kwa watu hao waliozuiliwa kurejeshwa makwao juzi Jumatano, Rubio alisema Trump "amehimiza" wafanyakazi hao kubaki Marekani ili kuendelea na kazi zao na kuwafunza wafanyakazi wenyeji walioajiriwa, shirika hilo la habari la Yonhap limeripoti.
Wachambuzi wameonya kuwa msako huo unaweza kuzuia kampuni za kigeni kuwekeza nchini Marekani. Kiwango cha uwekezaji wa kigeni katika miradi ya viwanda ya Marekani, ikiwa ni pamoja na ile inayoongozwa na kampuni za Korea Kusini, inahitaji wafanyakazi wenye ujuzi zaidi kuliko mipango ya sasa ya visa inavyoruhusu.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma