

Lugha Nyingine
SINOPEC yazindua programu ya mafunzo kwa Waganda zaidi ya 800
Washiriki mafunzo wakiangalia mashine wakati wa hafla ya ufunguzi wa programu ya kienyeji ya mafunzo ya ujuzi kwa wafanyakazi ya kampuni tanzu ya SINOPEC-Uganda kwenye Taasisi ya Mafunzo ya Mafuta na Gesi ya Sunmaker mjini Kampala, Uganda, Aprili 23, 2025. (Hajarah Nalwadda/Xinhua)
KAMPALA — SINOPEC, kampuni ya China iliyopewa kandarasi ya kujenga Kituo Kikuu cha Uchakataji Mafuta (CPF) nchini Uganda, imeanza kutoa mafunzo kwa Waganda zaidi ya 800 jana Jumatano, ikiwa ni sehemu ya juhudi za kuendeleza nguvukazi ya kienyeji yenye ujuzi kwa ajili ya sekta ya mafuta ya nchi hiyo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na SINOPEC, mafunzo hayo yatafanyika kwa makundi hadi Oktoba katika Taasisi ya Mafunzo ya Mafuta na Gesi ya Sunmaker, huku kozi zake zikijumuisha nyanja mbalimbali kama vile utengenezaji, uungaji mabomba na ufungaji wa nyenzo za kujengea (scaffolding).
Betty Jackie Namubiru, meneja wa maudhui ya kitaifa katika Mamlaka ya Mafuta ya Uganda, shirika la serikali linalosimamia sekta ya mafuta, amesema kuwa sekta hiyo bado inahitaji idadi kubwa ya wafanyakazi wenyeji wenye ujuzi.
"Kwahiyo ninataka kutumia fursa hii kuishukuru kampuni ya SINOPEC-Uganda kwa jitihada hii, na Sunmaker kwa juhudi ambazo wameweka kujenga mara kwa mara uwezo kwa Waganda," amesema Namubiru.
Yi Xuhui, mkurugenzi mradi wa SINOPEC, amesema kuwa kampuni hiyo tayari imetoa mafunzo kwa angalau watu 900 na inapanga kutoa mafunzo kwa wengine takriban 860 zaidi, hasa katika uchomeleaji wa mabomba, ufungaji wa CPF, ujenzi na matengenezo.
"Tupo hapa Uganda kwa ajili ya Uganda. Mafunzo yataendelea, na ujuzi huu unaotambulika kimataifa unaweza kutumiwa na washiriki popote duniani," amesema Yi.
Uganda iligundua akiba ya mafuta yenye kujaza mapipa bilioni 6.5 mwaka 2006, miongoni mwake mafuta ya mapipa bilioni 1.4 yanachukuliwa kuwa yanafaa kibiashara, kwa mujibu wa Wizara ya Nishati na Maendeleo ya Madini. Nchi hiyo kwa sasa inajenga kiwanda cha kusafisha mafuta na bomba la kusafirisha mafuta ghafi kama sehemu ya mkakati wake mpana wa maendeleo ya sekta ya mafuta.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma