

Lugha Nyingine
IMF yashusha makadirio ya ukuaji wa uchumi duniani hadi asilimia 2.8 mwaka 2025 huku kukiwa na ongezeko la ushuru
Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu Mtazamo wa Uchumi Duniani (WEO) mjini Washington, D.C., Marekani, Aprili 22, 2025. (Xinhua/Xie E)
WASHINGTON - Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) limepunguza makadirio yake ya ukuaji wa uchumi duniani mwaka 2025 hadi asilimia 2.8, ikiwa ni punguzo kubwa la asilimia 0.5 kutoka makadirio yake ya Januari, kwa mujibu wa Mtazamo Mpya wa Uchumi Duniani (WEO) uliotolewa jana Jumanne mjini Washington, D.C., Marekani.
"Tangu kutolewa kwa ripoti ya WEO ya Januari, Marekani imetangaza na kutekeleza hatua mbalimbali mpya za ushuru na wenzi wake wa kibiashara pia wamechukua hatua za kulipiza, hali ambayo imesababisha ushuru wa Marekani kwa nchi karibu zote duniani umetekelezwa Aprili 2 na kuvifanya viwango vya ushuru kufikia viwango ambavyo havijaonekana katika miaka mia moja iliyopita," ripoti hiyo imesema.
Ikisema kuwa ushuru wenyewe ni "mshtuko mkubwa mbaya," IMF imesema kuwa "hali ya kutotabirika" ambayo hatua hizi zimeleta kumeathiri vibaya shughuli za kiuchumi na mtazamo huo.
"Mfumo wa uchumi wa kimataifa ambao nchi nyingi zimekuwa zikijiendesha chini yake kwa miaka 80 iliyopita unaundwa upya, ikiingiza dunia katika zama mpya. Sheria zilizopo zinapingwa wakati mpya bado hazijajitokeza," Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Chini ya makadirio hayo yanayojumuisha taarifa kuanzia Aprili 4, ukuaji wa kimataifa unatarajiwa kushuka hadi asilimia 2.8 mwaka 2025 na asilimia 3 mwaka 2026 – chini kutoka asilimia 3.3 kwa miaka yote miwili kwenye ripoti ya WEO iliyotolewa Januari, na chini sana ya wastani wa kihistoria (2000-2019) wa asilimia 3.7, kwa mujibu wa ripoti hiyo mpya ya WEO.
Mchumi Mkuu wa IMF Pierre-Olivier Gourinchas (wa kwanza, kushoto) akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari kuhusu Mtazamo wa Uchumi Duniani (WEO) mjini Washington, D.C., Marekani, Aprili 22, 2025. (Xinhua/Xie E)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma