Lugha Nyingine
Ujumbe wa Iran watoka nje ya mazungumzo ya Uswisi kutokana na tishio jipya la mashambulizi la Trump

Maafisa wa polisi wakitembea kutoka nje ya hoteli kwenye kituo cha habari, Burgenstock karibu na Lucerne, Uswisi, Juni 21, 2026. (Xinhua/Lian Yi)
TEHRAN - Ujumbe wa Iran uliondoka kwenye mazungumzo na Marekani nchini Uswisi jana Jumapili kupinga tishio la Rais wa Marekani Donald Trump la kuanzisha mashambulizi zaidi dhidi ya Iran, shirika la habari la Tasnim la Iran limeripoti.
Shirika hilo limerejelea chanzo kilicho karibu na ujumbe huo kikisema kwamba "mazungumzo yamesimama dakika chache zilizopita."
Wakati huo huo, Press TV ya serikali ya Iran imekinukuu chanzo kikisema kwamba ujumbe huo uliwasilisha mapingamizi moja kwa moja kwa upande wa Marekani, na "unatathmini hali ili kutoa jibu mwafaka" kwa tishio hilo la Trump.
Mapema siku hiyo, Trump aliandika kwenye Truth Social: "Iran lazima izuie mara moja VIBARAKA wao wanaolipwa sana nchini Lebanon ili wasisababishe matatizo. Wasipofanya hivyo, tutaipiga Iran vikali tena, kama tu tulivyofanya wiki iliyopita, ila vikali zaidi!!!"
Spika wa Bunge la Iran Mohammad Bagher Ghalibaf, ambaye anaongoza ujumbe huo, alipinga tishio hilo, akisema vikosi vya Iran viko tayari kukabiliana.
"Ni bora wawe waangalifu kuhusu maoni yao ... Chochote wanachosema, sisi ndio tunaochukua hatua," amesema.
Mazungumzo hayo nchini Uswizi yanalenga kutekeleza Kifungu cha 13 cha nyaraka ya makubaliano kati ya Iran na Marekani (MoU) iliyosainiwa hivi karibuni, ambacho kinaweka mazingira ya kuanzisha mazungumzo ya makubaliano ya mwisho, ikihusisha kukomesha vita katika pande zote ikiwemo Lebanon, kuondoa kizuizi cha majini cha Marekani, kufungua tena Mlango-Bahari wa Hormuz, kutoa msamaha kwa mauzo ya nje ya mafuta ya Iran, na kuziachilia mali za Iran zilizozuiliwa, shirika la habari la Fars la Iran limeripoti Jumapili, likimrejelea Hossein Ghorbanzadeh, mjumbe wa ujumbe huo.
“Vifungu vingine katika MoU havitatekelezwa hadi vita nchini Lebanon vitakapoisha,” Ghorbanzadeh amesema, akiongeza kuwa rasimu ya msamaha wa vikwazo vya muda unaohusu mauzo ya nje ya mafuta na mali za Iran imekamilika na itaanza kutekelezwa hivi karibuni
MoU hiyo, iliyosainiwa kidijitali Alhamisi, ilifuatiwa na makubaliano ya kusimamisha mapigano kati ya Lebanon na Israeli ambayo yalianza kutekelezwa Ijumaa alasiri.
Siku ya Jumamosi, Waziri Mkuu wa Israeli Benjamin Netanyahu na Waziri wa Ulinzi Israel Katz waliripotiwa kuamuru jeshi kusimamisha mapigano nchini Lebanon. Lakini Katz alisema baadaye Jumapili kwamba jeshi halitajiondoa kutoka "ukanda wa usalama" linaoushikilia kusini mwa Lebanon.
Wakati huo huo, vyanzo vya habari nchini Lebanon vimeripoti kuendelea kwa mashambulizi ya Israeli dhidi ya Lebanon katika siku chache zilizopita licha ya tangazo hilo la kusimamisha mapigano.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



