M23 yadai kujiondoa kutoka mji muhimu wa Uvira mashariki mwa DRC huku serikali ikikanusha hatua hiyo

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Januari 19, 2026

Askari wa kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) wakionekana mjini Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 17, 2026. (Str/Xinhua)

Askari wa kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) wakionekana mjini Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 17, 2026. (Str/Xinhua)

KINSHASA - Kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) limetangaza kwamba litajiondoa kikamilifu kutoka mji wa Uvira, mji muhimu mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), ingawa serikali ya nchi hiyo imekuwa ikikanusha madai hayo mara kwa mara.

Msemaji wa M23 Lawrence Kanyuka alisema Jumamosi kuwa kundi hilo limechukua "uamuzi mgumu" wa kuondoa vikosi vyake, akiongeza kuwa mji wa Uvira utawekwa "chini ya wajibu kamili wa Umoja wa Mataifa na jumuiya ya kimataifa."

Alisema hatua hiyo inalenga kutoa nafasi kwa juhudi zinazoendelea za amani za kikanda kufanikiwa, ingawa hakutaja idadi ya wapiganaji waliohusika.

Mwezi Desemba 2025, kundi hilo lilisema lilianza kujiondoa kutoka Uvira, mji muhimu katika Jimbo la Kivu Kusini ambao lilikuwa limeuteka hapo awali, likiielezea hatua hiyo kuwa ni ishara ya nia njema ya kuunga mkono juhudi za amani.

Hata hivyo, serikali ya DRC imekuwa ikikanusha madai hayo mara kwa mara. Akizungumza Jumamosi jioni, msemaji wa serikali Patrick Muyaya alitupilia mbali tangazo hilo, akilielezea kuwa "halina na maana," na kuliita kuwa ni "mbinu ya upotoshaji."

"Kujiondoa bila kuondoka ni nini?" Muyaya alihoji, akionya kwamba waasi hao wanaweza kuwaacha wapiganaji waliopenyezwa. Amesisitiza kwamba serikali itatambua tu kujiondoa huko mara tu mamlaka ya serikali na huduma za umma zitakaporejeshwa kikamilifu.

Mji wa Uvira, ulioko kwenye mwambao wa Ziwa Tanganyika karibu na mpaka wa Burundi, umekuwa ukitumika kama kituo cha muda cha kiutawala cha jimbo la Kivu Kusini baada ya mji mkuu wa jimbo hilo, Bukavu, kutekwa na M23 mwezi Februari 2025.

Mapigano yameendelea katika siku za hivi karibuni kwenye maeneo kadhaa karibu na Uvira, yakionyesha hali inayoendelea ya ukosefu wa utulivu mashariki mwa DRC.

M23 ilisema Alhamisi wiki iliyopita kwamba imeomba MONUSCO kulinda raia wa Uvira kwa mujibu wa majukumu yake, ingawa ujumbe huo bado haujatoa majibu.

Eneo la Mashariki mwa DRC limekumbwa na miongo kadhaa ya migogoro ya silaha, hali ambayo imezidishwa zaidi na kurejea kwa uasi wa M23 tangu mwishoni mwa mwaka 2021.

Askari wa kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) wakionekana mjini Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 17, 2026. (Str/Xinhua)

Askari wa kundi la waasi la Vuguvugu la Machi 23 (M23) wakionekana mjini Uvira, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), Januari 17, 2026. (Str/Xinhua)

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Zhao Jian)

Picha