Japan lazima ifanye tafakari ya kina kuhusu uhalifu wake wa kihistoria: Mjumbe wa China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 19, 2025

UMOJA WA MATAIFA - Japan, ikiwa nchi iliyoshindwa kwenye Vita vya Pili vya Dunia, lazima ifanye tafakari ya kina juu ya uhalifu wake wa kihistoria, iheshimu ahadi za kisiasa ilizotoa kuhusu suala la Taiwan, iache mara moja vitendo vya uchochezi vinavyovuka mstari, na irejeshe kauli zake zisizo sahihi. Hayo yamesemwa na mjumbe wa kudumu wa China katika Umoja wa Mataifa Fu Cong Alhamisi kwenye mkutano wa ngazi ya juu wa wajumbe wote wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa ya kuadhimisha siku ya kwanza ya Kimataifa ya Kupinga Ukoloni katika Aina na Udhihirisho wake Wote.

Mjumbe huyo amesema dunia bado haijaondokana kikamilifu na kivuli cha ukoloni, licha ya kumalizika kwa utawala wa kikoloni na kuporomoka kwa mifumo ya kikoloni.

Ameihimiza jumuiya ya kimataifa kupinga vikali maneno au vitendo vyovyote vinavyodhoofisha au kutishia kuvuruga utaratibu wa kimataifa wa baada ya vita.

Balozi Fu amesema kuwa Siku ya Kimataifa ya Kupinga Ukoloni katika Aina na Udhihirisho wake Wote inalenga kuhimiza jumuiya ya kimataifa kukumbuka madhara ya ukoloni, kuharakisha mchakato unaoendelea wa kuondoa ukoloni, na kukomesha ukoloni katika aina na udhihirisho wake wote.

"Historia ya Vita vya Kupinga Ufashisti Duniani inatufundisha kwamba amani inahitaji kupiganiwa kwa juhudi na kulindwa," Balozi Fu amesema.

Amesema baada ya ushindi wa Vita vya Pili vya Dunia, kesi za wahalifu wa vita katika Mahakama ya Kimataifa ya Kijeshi ya Nuremberg na Mahakama ya Kimataifa ya Kijeshi ya Mashariki ya Mbali zilihakikisha kwamba wahusika wakuu wa vita vya uvamizi, ambao mikono yao ilikuwa imetiwa doa la damu ya watu wa mataifa mengi, waliadhabiwa ipasavyo.

"Haki na uadilifu wa kesi hizo hautikisiki na hauwezi kupingwa," amesema.

Balozi Fu amesema kuwa katika historia, Japan ilivamia China, Penninsula ya Korea na Asia ya Kusini na Mashariki, na kulazimisha utawala wa kikatili wa kikoloni.

Amesema kuwa wavamizi wa Japan walifanya uhalifu na ukatili mwingi katika Taiwan, kuua zaidi ya watu 650,000, kuajiri kwa nguvu takriban vijana 200,000 kutumikia jeshini, na kulazimisha wanawake zaidi ya 2,000 wa Taiwan kuwa "wanawake waliolazimishwa kutoa huduma za kijinsia," kutwaa asilimia 70 ya ardhi ya Taiwan, na kuchimba vibaya rasilimali asilia, zikiwemo migodi ya makaa ya mawe na dhahabu.

"Hatupaswi kamwe kuruhusu kukataliwa au kupotoshwa kwa aina yoyote historia ya uvamizi, kamwe hatupaswi kuruhusu kufufuliwa kwa umilitarizm (militarism), na kamwe hatupaswi kuruhusu kujirudia kwa maafa ya kihistoria," mjumbe huyo wa China amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Renato Lu)

Picha