Vikundi vya mrengo wa kulia vya Japan vina desturi ya kubuni simulizi za uongo: Msemaji

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Desemba 18, 2025

BEIJING – Vikundi vya mrengo wa kulia vya Japan vina tabia ya kubuni simulizi za uongo, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun amesema jana Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari alipoulizwa kutoa maoni yake kuhusu madai ya baadhi ya watu wa Japan kwamba Japan ni nchi "inayopenda amani" na kwamba shutuma za China "haziendani na ukweli wa mambo."

"Kile ambacho upande wa Japan umesema na kufanya ni mfano mwingine wa namna baadhi ya watu nchini Japan wanavyopotosha ukweli wa mambo kwa makusudi, kukataa kurekebisha makosa yao, na kujaribu kujifanya hawana hatia ili kujipatia huruma kutoka kwa jumuiya ya kimataifa," Guo amesema, akiongeza kuwa si mara ya kwanza kwa vikundi hivyo vya mrengo wa kulia nchini Japan kubuni simulizi za uongo.

Guo amesema vikundi hivyo vya mrengo wa kulia vilielezea vita vya uvamizi wa Japan dhidi ya majirani wa Asia kuwa ni "ukombozi wa Asia," vilipunguza uzito wa Mauaji ya Halaiki ya Nanjing kwa kuyaita "tukio la Nanjing," vilikisafisha Kitengo maarufu cha 731 kuwa "kitengo cha utafiti wa afya ya umma," na kuvifanyia upotoshaji masuala ya kazi ya kulazimishwa na "wanawake waliolazimishwa kutoa huduma za kijinsia" kwa kuyataja kuwa "vitendo vya hiari".

"Baada ya vita, Japan imejielezea yenyewe kuwa ni "mwathirika" wa vita huku ikiepuka kutaja kwamba umilitarizm (militarism) ndiyo hasa chanzo cha vita," Guo amesema.

Amesema Japan inadai kushikilia kanuni inayolenga ulinzi pekee na mkakati wa ulinzi usio wa kushambulia, lakini imerahisisha vizuizi katika kutekeleza haki ya kujilinda kwa pamoja, imeendelea kulegeza vizuizi vya uuzaji nje wa silaha, na hata kujaribu kurekebisha kanuni zake tatu za kutokuwa na nyuklia.

Amesema kuwa kauli potofu za Waziri Mkuu wa Japan Sanae Takaichi kuhusu Taiwan zimepokelewa na hasira za watu wa China pamoja na upingaji na ukosoaji kutoka Japan na baadhi ya nchi nyingine.

"Kile ambacho upande wa Japan unapaswa kufanya ni kusikiliza miito hii na kufanya kujitafakari kwa kina badala ya kujitihada zisizo na tija za kushawishi nchi nyingine kuamini maelezo yao yasiyo na msingi," Guo amesema.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha