Lugha Nyingine
China yatoa vibali vya kwanza kwa magari ya kujiendesha ya ngazi ya 3
Mtembeleaji (wa kwanza, kulia) akifahamishwa kuhusu gari linalojiendesha lenyewe lenye Mfumo wa Satalaiti ya Urambazaji wa BeiDou (BDS) kwenye Mkutano wa 4 wa Kimataifa kuhusu Matumizi ya BDS mjini Zhuzhou, Mkoa wa Hunan, katikati mwa China, Septemba 24, 2025. (Xinhua/Chen Sihan)
BEIJING - China imetoa idhini kwa usafiri wa magari ya aina mbili ya sedan ya kutumia umeme yaliyowekwa mfumo wa uwezo wa kujiendesha yenyewe wa Ngazi ya 3, hii ni mara ya kwanza kuruhusu magari ya aina hiyo kujiendesha kwenye barabara za kiumma.
Aina hizo mbili za magari zimeundwa na kampuni za kuunda magari za Changan na Arcfox ya Kampuni ya Magari ya BAIC, taarifa iliyotolewa na Wizara ya Viwanda na Teknolojia ya Upashanaji Habari ya China (MIIT) imeeleza.
Taarifa hiyo imesema, gari hilo la Changan lina uwezo wa kujiendesha lenyewe kwenye njia moja ya kupitisha magari kwa kasi ya hadi kilomita 50 kwa saa wakati wa msongamano barabarani, na limeidhinishwa kuendeshwa kwenye sehemu teule za barabara za mwendokasi na za barabara kuu za mijini katika Mji wa Chongqing, kusini magharibi mwa China.
Imeeleza kwa gari hilo la Arcfox linaruhusiwa kujiendesha lenyewe kwa kasi ya hadi kilomita 80 kwa saa kwenye sehemu maalum za barabara za mwendokasi na barabara kuu za mijini katika mji wa Beijing.
Mfumo wa gari la kujiendesha lenyewe umegawanywa katika ngazi sita kuanzia Ngazi ya 0 hadi Ngazi ya 5. Kadiri ngazi inavyozidi kuwa ya juu, ndivyo teknolojia husika inavyokuwa ya hali ya juu na yenye akili zaidi. Ngazi hiyo ya 3, ya "kujiendesha kwa kujitegemea kwa masharti," huruhusu magari kufanya kazi za kujiendesha wakati huohuo ikimtaka dereva binadamu kuendelea kuwepo kwa utayari wa kuchukua udhibiti anapoombwa.
Katika miaka ya hivi karibuni, China imekuwa ikihimiza matumizi ya magari ya kujiendesha yenyewe. Mwezi Septemba, nchi hiyo ilitoa mpango kazi unaoelezea idhini ya masharti kwa ajili ya uundaji wa magari ya Ngazi hiyo ya 3.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



