Lugha Nyingine
Uzalishaji na Mauzo ya China ya Magari yanayotumia Nishati Mpya vyaongezeka katika miezi 10 ya kwanza ya 2025

Picha hii iliyopigwa Novemba 3, 2025 ikionyesha mstari wa kuunganisha magari yanayotumia nishati mpya (NEV) wa BYD, kampuni kubwa ya NEV ya China, kwenye kiwanda cha BYD mjini Zhengzhou, Mkoani Henan, katikati mwa China. (Xinhua/Li Jianan)
BEIJING - Sekta ya magari yanayotumia nishati mpya (NEV) ya China imeonyesha ukuaji mkubwa katika uzalishaji na mauzo katika kipindi cha miezi 10 ya kwanza ya mwaka 2025, kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa jana Jumanne na Jumuiya ya Wazalishaji wa Magari ya China (CAAM).
Takwimu hizo za CAAM zinaonesha kuwa uzalishaji wa magari hayo umeongezeka kwa asilimia 33.1 kulinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia magari karibu milioni 13.02 katika kipindi cha miezi 10 hiyo ya kwanza.
Aidha, takwimu hizo zinaonesha kuwa mauzo katika kipindi hicho yaliongezeka kwa asilimia 32.7 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia magari zaidi ya milioni 12.94, ikichukua asilimia 46.7 ya jumla ya mauzo yote ya magari mapya nchini China.
Kwa mujibu wa jumuiya hiyo, soko la magari la China lilidumisha mwelekeo wa ukuaji imara mwezi Oktoba, huku soko la magari yanayotumia nishati mpya likikua kwa kasi na mauzo ya magari nje ya nchi yakionyesha kuimarika.
Takwimu za jumuiya hiyo zinaonesha kuwa, mwezi Oktoba pekee, mauzo ya magari hayo yanayotumia nishati mpya yalifikia magari karibu milioni 1.72, yakichukua asilimia 51.6 ya mauzo yote ya magari mapya ya China. Jumuiya hiyo imeeleza kuwa, hali hiyo pia inaonyesha mara ya kwanza kwa mauzo hayo kuzidi nusu ya mauzo yote ya magari mapya nchini China.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa, jumla ya magari yaliyozalishwa China ilizidi magari milioni 27.69 katika miezi 10 hiyo ya kwanza, ikionyesha ongezeko la asilimia 13.2 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana, wakati huohuo mauzo yaliongezeka kwa asilimia 12.4 hadi kufikia magari karibu milioni 27.69.
Takwimu hizo za Jumanne pia zinaonyesha kuwa mauzo ya nje ya magari ya China yaliongezeka kwa asilimia 15.7 ikilinganishwa na mwaka jana hadi kufikia magari milioni 5.62 katika kipindi hicho hicho. Hasa mauzo ya nje ya magari yanayotumia nishati mpya yaliongezeka kwa asilimia 90.4 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka jana hadi kufikia magari milioni 2.01.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



