Umoja wa Mataifa watahadharisha kuhusu msukosuko wa kibinadamu unaozidi kuongezeka nchini Madagascar

(CRI Online) Novemba 05, 2025

Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Farhan Haq, amesema kuwa Madagascar inakabiliwa na msukosuko wa kibinadamu unaozidi kuzorota, hasa katika mikoa ya Grand Sud na Grand Sud-Est, ambayo ilikumbwa na mfululizo wa ukame, vimbunga na majanga mengine mwaka huu na mwaka jana.

Akirejelea Ofisi ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa (OCHA), msemaji huyo amewaambia wanahabari jana Jumanne kwenye makao makuu ya Umoja wa Mataifa kuwa athari endelevu za ukame wa El Nino na msimu wa kimbunga, zikichangamana na mlipuko wa malaria na mifumo dhaifu ya afya, vimesababisha jamii nyingi nchini humo kukosa uwezo wa kurejea katika hali ya kawaida.

Amesema, idadi ya watu wanaokabiliwa na dharura ya hali ya ukosefu wa usalama wa chakula katika mkoa wa Grand Sud inakadiriwa kuongezeka mara nne hadi laki 1.1 ifikapo mwezi Januari mwaka kesho, na kwamba visa vya watu wenye hali ya utapiamlo mkali mkoani humo viliongezeka mwaka jana, ikiathiri watoto karibu laki 1.6.

(Wahariri wa tovuti:Liu Mengxue,Renato Lu)

Picha