Lugha Nyingine
Wakuu wa serikali za China na Russia wafanya mkutano, wakitazamia ushirikiano wa karibu zaidi wa pande zote

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akiongoza mkutano wa 30 wa kawaida wa wakuu wa serikali za China na Russia pamoja na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin mjini Hangzhou, Mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, Novemba 3, 2025. (Xinhua/Huang Jingwen)
HANGZHOU - Waziri Mkuu wa China Li Qiang jana Jumatatu wakati akiongoza mkutano wa 30 wa kawaida wa wakuu wa serikali za China na Russia pamoja na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin mjini Hangzhou, mji mkuu wa Mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China, ameelezea nia ya China ya kushirikiana na Russia katika kuzidisha ushirikiano kwenye nyanja zote ili kulinda maslahi yao ya pamoja ya maendeleo na usalama kwa namna iliyoboreshwa.
Mkutano huo wa kawaida, ambao umekuwa ukifanyika kila mwaka tangu kuanzishwa kwake mwaka 1996, ni utaratibu muhimu wa kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa kati ya wakuu wa nchi hizo mbili, na kuhimiza ushirikiano wa pande mbili na mabadilishano ya kati ya watu.
Li amesema kwamba mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 80 tangu kupatikana ushindi katika Vita vya Watu wa China vya Kupambana na Uvamizi wa Japan, Vita Vikuu ya Kizalendo vya Umoja wa Kisovieti na Vita vya Dunia vya Kupinga Ufashisti na kwamba nchi hizo mbili zimeungana mkono katika kufanya shughuli kubwa za kumbukumbu, zikiimarisha urafiki wao zaidi.
Amesema kwamba China ina nia ya kushirikiana na Russia ili kutumia makubaliano muhimu yaliyofikiwa kati ya wakuu wao wawili wa nchi kama mwongozo wa kimsingi, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati, kuzidisha ushirikiano katika nyanja mbalimbali, na kulinda maslahi ya pamoja ya maendeleo na usalama kwa namna iliyoboreshwa.
"Mwezi uliopita, mkutano wa nne wa wajumbe wote wa Kamati Kuu ya 20 ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ulijadili na kupitisha mapendekezo kwa ajili ya uundaji wa Mpango wa 15 wa Miaka Mitano wa nchi hiyo – dira ya maendeleo ya China katika miaka mitano ijayo na zaidi," Li amesema.
Amesisitiza kwamba China ina nia ya kushirikiana na Russia ili kuungana mkono kithabiti, kuboresha mawasiliano ya ngazi ya juu, kuimarisha kuendana kimkakati, kupanua ushirikiano katika nyanja mbalimbali, kusukuma kila wakati ushirikiano wa kimkakati wa pande zote wa uratibu kati ya China na Russia kwa zama mpya, na kuendelea kusonga mbele bega kwa bega katika njia ya kujenga mambo ya kisasa.
Kwa upande wake, Mishustin amesema kwamba ushirikiano wa kimkakati wa pande zote wa uratibu katika zama mpya kati ya Russia na China kwa sasa uko katika ngazi yake ya juu zaidi kihistoria.
"Russia ina nia ya kuboresha mawasiliano yake ya ngazi ya juu na China, kuandaa shughuli mbalimbali za Mwaka wa Utamaduni kati ya Russia na China, kuimarisha kila wakati mambo ya uhusiano wa pande mbili, na kupanua ushirikiano na mabadilishano katika sekta kama vile biashara, uwekezaji, uchukuzi, nishati, kilimo, utamaduni na uchumi wa kidijitali," amesema.

Waziri Mkuu wa China Li Qiang akiongoza mkutano wa 30 wa kawaida wa wakuu wa serikali wa China na Russia pamoja na Waziri Mkuu wa Russia Mikhail Mishustin mjini Hangzhou, Mkoani Zhejiang, mashariki mwa China, Novemba 3, 2025. (Xinhua/Gao Jie)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma



