China yatangaza matokeo ya mazungumzo ya uchumi na biashara kati ya China na Marekani mjini Kuala Lumpur

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Oktoba 31, 2025

BEIJING - Wizara ya Biashara ya China jana Alhamisi ilitangaza matokeo yaliyopatikana na wajumbe wa China na Marekani kwenye mazungumzo yao ya uchumi na biashara yaliyofanyika hivi karibuni mjini Kuala Lumpur, Malaysia.

Wizara hiyo imesema kwamba, Marekani itafuta kile kinachoitwa "ushuru wa fentanyl" wa asilimia 10 na kusimamisha kwa mwaka mmoja, ushuru wa kutozana sawa wa asilimia 24 unaotozwa kwa bidhaa za China, zikiwemo bidhaa kutoka Mikoa ya Utawala Maalum ya Hong Kong na Macao ya China.

"China itafanya marekebisho sawia kwenye hatua zake za kulipiza dhidi ya ushuru uliotajwa hapo juu wa Marekani," msemaji wa wizara hiyo amesema, akiongeza kuwa pande zote mbili zimekubaliana kuendelea kuongeza muda wa hatua fulani za ushuru.

Amesema, Marekani itasimamisha kwa mwaka mmoja utekelezaji wa sheria mpya iliyotangazwa Septemba 29 ambayo inapanua "orodha yake ya mashirika" yaliyowekewa vizuizi vya kuuza nje kwa shirika au kampuni yoyote ambayo inamilikiwa kwa angalau asilimia 50 na shirika au kampuni moja au zaidi kwenye orodha hiyo wakati huohuo China itasimamisha utekelezaji wa hatua husika za kudhibiti uuzaji nje zilizotangazwa Oktoba 9 kwa mwaka mmoja na itapitia na kuboresha mipango husika.

"Marekani itasimamisha utekelezaji wa hatua chini ya uchunguzi wake wa Kifungu cha 301 unaolenga mambo ya baharini, uchukuzi wa bidhaa na viwanda vya ujenzi wa meli vya China kwa mwaka mmoja" amesema, akiongeza kuwa katika kukabiliana na hali hiyo, China itasimamisha utekelezaji wa hatua zake za kulipiza dhidi ya Marekani kwa mwaka mmoja mara tu usimamishaji huo wa Marekani utakapoanza kufanya kazi.

“Aidha, pande hizo mbili pia zimefikia maafikiano kuhusu masuala kadhaa yakiwemo ya ushirikiano wa kupambana na dawa za kulevya zinazotokana na fentanyl, kupanua biashara ya bidhaa za kilimo, na kushughulikia masuala yanayohusu kampuni husika,” msemaji huyo ameeleza.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha