

Lugha Nyingine
Rais wa zamani wa DRC Kabila ahukumiwa kifo bila mwenyewe kuwepo
Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo DRC Joseph Kabila amehukumiwa kifo bila mwenyewe kuwepo mahakamani na Mahakama Kuu ya Kijeshi ya nchi hiyo kwa makosa kadhaa yakiwemo uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.
Kwa mujibu wa hukumu hiyo, Kabila amekutwa na hatia kwa makosa kadhaa, kama vile kushiriki katika harakati za uasi, mauaji ya makusudi, mateso, ubakaji na kuchukua kwa nguvu udhibiti wa Goma, mji mkuu wa Jimbo la Kivu Kaskazini, ambao sasa unashikiliwa na waasi wa kundi la M23.
Kabila pia amepokea kifungo cha miaka 15 jela kwa kosa la kula njama, wakati mahakama hiyo ikitangaza hukumu ya kifo kwa makosa hayo mengine.
Kesi yake, iliyoanza kusikilizwa mwezi Julai baada ya Baraza la Seneti la DRRC kumuondolea Kabila kinga ya kutoshtakiwa mwezi Mei, iliendeshwa bila mshtakiwa huyo kuwepo mahakamni.
Mwendesha mashtaka alimshutumu rais huyo wa zamani kwa kuhusika na vitendo vya ukatili vilivyofanywa na M23 katika majimbo ya mashariki. Ushahidi uliowasilishwa ulijumuisha maelezo ya mashuhuda, picha za video, na mahojiano ya vyombo vya habari.
Kabila, aliyetawala nchi hiyo kuanzia mwaka 2001 hadi 2019, amekuwa akiishi Afrika Kusini tangu 2023.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma