

Lugha Nyingine
China yapendekeza mpango wa ushirikiano wa mtandao kwenye jukwaa la intaneti la China na Afrika
XIAMEN - Baraza la Maendeleo na Ushirikiano wa Intaneti la China na Afrika limefunguliwa jana Jumapili katika Mji wa Xiamen, Mkoa wa Fujian, mashariki mwa China, huku China ikizindua mpango kazi wa kujenga jumuiya ya pamoja ya nafasi ya mtandao na kuzindua mtandao kwa kampuni za intaneti za China zinazofanya kazi barani Afrika.
Mpango huo uliopewa jina la "Mpango Kazi wa Kujenga kwa Pamoja Jumuiya ya China na Afrika yenye Mustakabali wa Pamoja katika Nafasi ya Mtandao (2025-2026)", umetangazwa kwenye ufunguzi wa baraza hilo. China pia imeahidi kuendelea kuwa mwenyeji wa programu za mafunzo juu ya usalama wa mtandao na uchumi wa kidijitali.
Baraza hilo, linajumuisha majukwaa madogo yanayojikita katika kuziba mgawanyiko wa kidijitali, uendelezaji na usimamizi wa AI, usalama wa mtandao na usimamizi wa data, na ushirikiano wa vyombo vya habari na mawasiliano kati ya watu na watu. Wawakilishi takriban 400 kutoka serikali, vyuo vikuu, taasisi za washauri bingwa na vyombo vya habari nchini China na nchi 32 za Afrika wanashiriki kwenye baraza hilo.
Washiriki wa Afrika wamepongeza mpango huo, wakilielezea baraza hilo kuwa linaendana na mahitaji ya mageuzi ya kidijitali barani Afrika. Wameelezea matumaini ya kuimarisha ushirikiano na China katika uchumi wa kidijitali, usalama wa mtandao, ulinzi wa data, usimamizi wa AI na mawasiliano ya vyombo vya habari.
Baraza hilo limeandaliwa kwa pamoja na Mamlaka ya Nafasi ya Mtandao ya China na serikali ya mkoa wa Fujian.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma