

Lugha Nyingine
Ripoti yaonesha biashara ya kidijitali duniani kufikia thamani ya dola za Kimarekani trilioni 7.23 huku ikiwa na ukuaji thabiti
Hafla ya uzinduzi wa Maonyesho ya 4 ya Biashara ya Kidijitali Duniani ikifanyika mjini Hangzhou, Mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China, Septemba 25, 2025. (Xinhua/Xu Yu)
HANGZHOU - Sekta ya biashara ya kidijitali duniani imeonyesha nguvu kubwa ya ukuaji, huku thamani ya mauzo ya nje ikipanda kutoka dola za Kimarekani trilioni 4.59 mwaka 2020 hadi dola za Kimarekani trilioni 7.23 mwaka 2024, ikifikia wastani wa ongezeko la asilimia 12.1 kwa mwaka, ripoti iliyotolewa Ijumaa katika Mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China imeonesha.
Kiwango hicho cha ukuaji kinapita kile cha biashara ya jumla duniani katika kipindi hicho, kikionesha dhahiri upanuzi wenye nguvu wa biashara ya kidijitali, imesema ripoti hiyo yenye kichwa cha "Ripoti ya Maendeleo ya Biashara ya Kidijitali Duniani 2025" iliyotolewa kwenye Maonyesho ya nne ya Biashara ya Kidijitali Duniani yanayoendelea mjini Hangzhou, mji mkuu wa mkoa huo.
Ripoti hiyo imeandaliwa kwa pamoja na Kituo cha Biashara ya Kimataifa (ITC) na kamati ya maandalizi ya maonyesho hayo.
Ripoti hiyo inaonyesha mazingira ya biashara ya kidijitali duniani yenye hali mbalimbali, huku Umoja wa Ulaya, Marekani, China, Uingereza na India zikiorodheshwa kuwa nchi tano kwenye nafasi za mbele.
Hasa, mauzo ya nje ya biashara ya kidijitali ya China mwaka 2024 yaliongezeka kwa asilimia 10.7 kuliko mwaka 2023 hadi kufikia dola za Kimarekani bilioni 793.7, yakisaidia kuchochea mazingira ya biashara ya kidijitali duniani kuelekea kuwa ya hali mbalimbali na uwiano zaidi.
Ripoti hiyo pia inatoa wito wa kuungwa mkono zaidi kwa kampuni ndogondogo, kampuni ndogo na za kati na wajasiriamali wanawake wanaojihusisha na biashara ya kidijitali. Utafiti wa ITC umeonesha kuwa wanawake katika nchi zinazoendelea bado wanakabiliwa na vizuizi katika biashara ya kimataifa, wakati biashara ya kidijitali inatoa fursa za ajira zenye unyumbufu , kuvunja vizuizi vya muda na vya kijiografia.
Robert Skidmore, anayesimamia uwezo wa ushindani wa sekta na kampuni katika ITC, ametoa wito wa kuzitaka serikali, kampuni na mashirika ya kimataifa kushirikiana katika kukuza uvumbuzi na kuhakikisha manufaa ya uchumi wa kidijitali yanamfikia kila mtu, hasa kampuni ndogondogo, kampuni ndogo na za kati katika nchi zinazoendelea.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma