Uingereza na Ujerumani zasaini mkataba wa ulinzi na uhamiaji

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Julai 18, 2025

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kushoto) akipeana mkono na Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz katika No. 10 Mtaa wa Downing mjini London, Uingereza, Julai 17, 2025. (Xinhua)

Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kushoto) akipeana mkono na Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz katika No. 10 Mtaa wa Downing mjini London, Uingereza, Julai 17, 2025. (Xinhua)

LONDON - Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer na Chansela wa Ujerumani Friedrich Merz wametia saini mkataba wa pande mbili kuhusu mambo mbalimbali yakiwemo ulinzi na uhamiaji, ambao unaaminika kuwa mkataba muhimu zaidi kati ya Uingereza na Ujerumani tangu kumalizika kwa Vita vya Pili vya Dunia.

Mkataba huo unajumuisha vipengele vya usalama na ulinzi vinavyozitaka nchi hizo mbili kufanya mazoezi na mafunzo ya pamoja ya kijeshi, kukabiliana na vitisho vya mtandaoni na vita vya habari, na kuratibu juu ya mauzo ya nje ya silaha.

Katika mkataba huo, nchi hizo mbili pia zimesisitiza tena dhamira yao ya kuzuia ongezeko la kiwango cha joto duniani lisizidi nyuzi joto 1.5 kuliko viwango vya kabla ya viwanda, ambayo imeendana na mambo husika katika Mkataba wa Paris wa kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi na athari zake mbaya.

Mkataba huo pia unaahidi kuimarisha biashara ya pande mbili ndani ya mfumo wa makubaliano ya Umoja wa Ulaya na Uingereza na dhamira kwa soko huria na wazi, vilevile kuongeza ajira na kukuza idadi ya fursa za kazi zenye ubora wa kiwango cha juu.

Ukiwa umepewa jina la Mkataba wa Kensington, Starmer amesema ni "wa kwanza wa aina yake kuwahi kutokea" kati ya nchi hizo mbili na ni ushahidi wa "ukaribu wa uhusiano wetu kama ulivyo leo."

Ameongeza kuwa mkataba huo unaonesha "uhusiano imara na wa karibu kati ya nchi hizo mbili katika kipindi chenye hali tete duniani." 

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha