

Lugha Nyingine
Trump asema Marekani kusafirisha silaha nchini Ukraine kupitia NATO, atishia "ushuru mkubwa" kuilenga Russia
WASHINGTON - Rais Donald Trump wa Marekani amesema kwamba Marekani itasafirisha silaha kwa Ukraine kupitia NATO, na kutishia kutoza "ushuru mkubwa" Russia kama makubaliano ya kusimamisha vita hayatafikiwa ndani ya siku 50.
Trump ametangaza makubaliano na NATO kuhusu silaha za kuisaidia Ukraine wakati akikutana na Katibu Mkuu wa NATO Mark Rutte kwenye Ofisi ya Oval katika Ikulu ya White House, jana Jumatatu.
"Tutakuwa tukiwatumia wao silaha na watakuwa wanazilipia," Trump amesema, akiongeza kuwa Marekani itaunda silaha hizo.
"Tutakwenda kutoza ushuru mkubwa zaidi kama hatutakuwa na makubaliano ndani ya siku 50," Trump amesema kuhusu Russia.
Trump amesema kutakuwa na "ushuru wa pili" wa takriban asilimia 100, vyombo mbalimbali vya habari vimeripoti.
Waziri wa Biashara wa Marekani Howard Lutnick amefafanua baadaye kwamba Trump anamaanisha "vikwazo vya kiuchumi" wakati alipotishia "ushuru wa pili" dhidi ya Russia kama haitafikia makubaliano ya kumaliza vita nchini Ukraine ndani ya siku 50, Gazeti la Washington Times limeripoti.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano huo wa Ofisi ya Oval, Trump amesema kuwa makubaliano hayo na washirika wa NATO yamekamilika na kupitishwa kikamilifu, Gazeti la The New York Times limeripoti.
"Tutawatumia silaha nyingi za kila aina.....Na watakuwa wakiwasilisha silaha hizo mara moja kwenye eneo, kwenye eneo la vita, maeneo tofauti ya vita, na watakuwa wakilipia kwa asilimia 100." Trump amesema.
Pia amewaambia waandishi wa habari kwamba baadhi ya mifumo ya makombora ya Patriot itawasili Ukraine ndani ya siku chache, shirika la habari la ABC limeripoti.
Trump amesema nchi za Ulaya ambazo zina mifumo hiyo ya kiulinzi ya Patriots zitaihamishia Ukraine na "itaanza kuwasili hivi karibuni," ABC imeongeza katika habari yake hiyo.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma