

Lugha Nyingine
Uingereza na Ufaransa zakubaliana kuratibu katika kuzuia silaha za nyuklia, kuanzisha mpango mpya wa uhamiaji
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kushoto) akimkaribisha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika Mtaa wa Downing No.10 mjini London, Uingereza, Julai 10, 2025. (Xinhua/Wu Lu)
LONDON - Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer jana Alhamisi kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika kambi ya kijeshi iliyoko Northwood, karibu na London, amesema kuwa Uingereza na Ufaransa zimetia saini Azimio la Northwood kuruhusu nchi hizo mbili kuratibu katika kuzuia silaha za nyuklia kwa mara ya kwanza.
Starmer amesema, makubaliano hayo yanalenga kumwonyesha maadui kwamba shambulizi lolote dhidi ya nchi yoyote kati yao litasababisha mwitikio kutoka kwa nchi zote mbili.
Kwa upande wake, Macron, ambaye alikuwa anatazamiwa kuhitimisha ziara ya kiserikali ya siku tatu nchini Uingereza baadaye jana Alhamisi, amesisitiza umuhimu wa ushirikiano wa ulinzi na usalama kati ya nchi hizo mbili, akisema kwamba nyakati zimebadilika barani Ulaya na ushirikiano kati ya Uingereza na Ufaransa "lazima ubadilike ipasavyo."
Akirejelea mgogoro wa Russia na Ukraine, Macron amesema Ulaya lazima iwe na uwezo wa kutegemea ushirikiano wa kimkakati kati ya Uingereza na Ufaransa, nchi mbili pekee zenye silaha za nyuklia barani Ulaya.
Taarifa kutoka ofisi ya waziri mkuu wa Uingereza, imesisitiza "tishio kubwa kwa Ulaya" ambalo litasababisha mwitikio wa pamoja wa nyuklia. "Adui yeyote anayetishia maslahi muhimu ya Uingereza au Ufaransa anaweza kukabiliwa na nguvu za vikosi vya nyuklia vya nchi hizo mbili," imesema.
Wakati huo huo, Uingereza na Ufaransa zinapanga kuagiza makombora ya hatari zaidi ya Storm Shadow na kuongeza silaha kama sehemu ya makubaliano mapya ya ulinzi, kwa mujibu na taarifa hiyo.
Kufuatia Mkutano wa kilele kati ya Uingereza na Ufaransa katika Mtaa wa Downing na mkutano wa mtandaoni wa "muungano wa uhiari", uliomjumuisha Rais Volodymyr Zelensky wa Ukraine, Starmer ametangaza kuwa makao makuu ya muungano huo mpya unaounga mkono Ukraine yataanzishwa mjini Paris.
Kuhusu suala la uhamiaji, viongozi hao wawili wamezindua mpango mpya wa "one in, one out" ili kupunguza uvukaji wa wahamiaji kwenye Mlango bahari wa Uingereza.
Chini ya mpango huo, pamoja na mambo mengine, wahamiaji wanaofika Uingereza kupitia boti ndogo "watazuiliwa na kurudi Ufaransa kwa muda mfupi," Starmer amesema.
Wote wawili Macron na Starmer wanakabiliwa na shinikizo linaloongezeka katika nchi zao kutoka kwa maoni ya mrengo wa kulia na ya wapinga uhamiaji. Akihutubia bunge la Uingereza siku ya Jumanne, Macron aliielezea changamoto ya uhamiaji kuwa "mzigo" kwa nchi zote mbili.
Ziara hiyo ya Macron ni safari ya kwanza ya kiserikali nchini Uingereza kufanywa na rais wa Ufaransa tangu mwaka 2008, na Macron ni mkuu wa nchi wa kwanza wa Umoja wa Ulaya kuzuru nchi hiyo tangu Brexit.
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kushoto) akimkaribisha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika Mtaa wa Downing No.10 mjini London, Uingereza, Julai 10, 2025. (Xinhua/Wu Lu)
Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer (kushoto) akimkaribisha Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa katika Mtaa wa Downing No.10 mjini London, Uingereza, Julai 10, 2025. (Xinhua/Wu Lu)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma