

Lugha Nyingine
Waziri Mkuu wa Malaysia ahimiza nchi za ASEAN kushikamana ili kukabiliana na utumiaji biashara kama silaha
Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim akihutubia Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki (ASEAN) mjini Kuala Lumpur, Malaysia, Julai 9, 2025. (Xinhua/Cheng Yiheng)
KUALA LUMPUR - Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki (ASEAN) inapaswa kushikamana ili kukabiliana na hali ya kutumia biashara ya kimataifa kama silaha na kuondoa usumbufu, na kushikilia msimamo wenye kanuni kuhusu biashara huria na ya wazi, Waziri Mkuu wa Malaysia Anwar Ibrahim amesema jana Jumatano katika hotuba yake ya ufunguzi wa Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa ASEAN.
Anwar pia amehimiza kuimarisha zaidi biashara na ushirikiano katika kanda hiyo, kama mkakati wa muda mrefu wa kukabiliana na athari sumbufu za ushuru unaowekwa na Marekani.
"Duniani kote, zana zilizotumika kuzalisha ukuaji sasa zinatumiwa kuweka shinikizo, kutenganisha na kuzuia. Ushuru, vizuizi vya mauzo ya nje, na vikwazo vya uwekezaji sasa vimekuwa nyenzo kali za uhasama wa siasa za kijiografia. Hii si dhoruba ya kupita. Ni hali mpya ya zama zetu," amesema.
"Tunapojitahidi kukabiliana na shinikizo za nje, tunahitaji kuimarisha misingi yetu ya ndani. Kufanya biashara zaidi miongoni mwetu, kuwekeza zaidi kati yetu, na kushikilia kusukuma mbele ushirikiano katika sekta zote. Kujenga uchumi wenye nguvu, uliounganishwa zaidi wa ASEAN ni jambo la kimkakati ambalo litaimarisha umuhimu na unyumbufu wetu kwa miongo kadhaa ijayo," ameongeza.
Anwar amesisitiza kuwa jumuiya hiyo haipaswi kupoteza mwelekeo wa utekelezaji wa sera ambazo zitanufaisha raia wa jumuiya hiyo, haswa katika mawasiliano, usalama wa chakula, kubadilisha muundo kuwa wa kidijitali, elimu, afya ya umma, na uwezo wa kuhimili tabianchi, ambayo yote yataimarisha nguvu za mshikamano za jumuiya hiyo na kuboresha maisha ya watu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia Mohamad Hasan amesema katika hotuba yake ya ufunguzi katika kikao cha wajumbe wote kwamba ASEAN lazima ifanye kazi kuimarisha zaidi mafungamano na uratibu ili kukabiliana na changamoto zinazoletwa na mabadiliko ya tabianchi na matukio mengine yanayosumbua.
"Mistari ya makosa ya siasa za kijiografia imeendelea kupasuka, hali ya kuaminiana kimkakati imepungua, na maeneo ya hatari yameongezeka ... ni lazima tuendelee kuwekeza na kuweka imani yetu katika mfumo wa kikanda na mfumo wa pande nyingi. Lazima tuendelee kutetea kanuni za haki, kutendeana kwa haki, usawa na njia za kibinadamu," ameongeza.
Malaysia ni mwenyeji wa Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa ASEAN na mikutano inayohusiana nao kuanzia tarehe 8 hadi tarehe 11 Julai, chini ya kaulimbiu ya uenyekiti wake wa 2025 wa ASEAN "Ujumuishaji na Uendelevu."
Waziri wa Mambo ya Nje wa Malaysia Mohamad Hasan akizungumza kwenye Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki (ASEAN) mjini Kuala Lumpur, Malaysia, Julai 9, 2025. (Xinhua/Cheng Yiheng)
Wahudhuriaji wakiwa katika picha ya pamoja kwenye Mkutano wa 58 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa Jumuiya ya Nchi za Asia Kusini-Mashariki (ASEAN) mjini Kuala Lumpur, Malaysia, Julai 9, 2025. (Xinhua/Cheng Yiheng)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma