

Lugha Nyingine
Wanaanga wa Shenzhou-19 wakutana na waandishi wa habari baada ya kurudi kutoka anga ya juu
Wanaanga Cai Xuzhe (katikati), Song Lingdong (kulia) na Wang Haoze waliotekeleza jukumu la chombo cha Shenzhou-19 cha China cha kubeba binadamu kufanya safari kwenye anga ya juu wakipiga saluti kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Julai 9, 2025. (Xinhua/Li Yanchen)
BEIJING - Wanaanga watatu Cai Xuzhe, Song Lingdong na Wang Haoze waliotekeleza jukumu la chombo cha kubeba binadamu cha Shenzhou-19 cha China kufanya safari kwenye anga ya juu wamekutana na waandishi wa habari mjini Beijing jana Jumatano, ikiwa ni mara yao ya kwanza kuonekana hadharani baada ya kurejea duniani mwezi Aprili, ambapo imeelezwa kuwa wanaanga hao wako katika afya njema ya kimwili na kiakili na matokeo yao ya vipimo vya afya yote yanaonesha hali ya kawaida.
Kwenye mkutano huo na waandishi wa habari, nguvu zao za misuli, uhimilivu na mazoezi ya ufanyaji kazi wa moyo na mishipa pia kimsingi vimeripotiwa kurudi kwenye viwango vya kabla ya safari yao hiyo ya anga ya juu.
Chombo cha anga ya juu cha Shenzhou-19 kilirushwa Oktoba 30, 2024 ikaunganishwa na chombo kikuu cha kituo cha anga ya juu cha China, Tianhe, na kuwa muundo mmoja. Wanaanga hao watatu walirejea duniani Aprili 30.
"Wakati wa siku 183 za safari ya kwenye obiti, tulikamilisha shughuli tatu za nje ya kituo (EVAs), kazi nyingi za uwasilishaji mizigo, majaribio na upimaji wa kisayansi kadhaa katika nyanja mbalimbali," amesema Cai, kamanda wa wanaanga hao wa Shenzhou-19, akiongeza kuwa kati ya miradi hiyo, mingi ilitekelezwa kwa mara ya kwanza tangu kituo cha anga ya juu cha China kilipoingia katika kipindi cha matumizi na uendelezaji.
Cai ameshiriki katika utekelezaji wa majukumu mawili ya vyombo vya anga ya juu vya Shenzhou-14 na Shenzhou-19. "Kila jukumu si marudio rahisi ya lile la awali, bali ni upigaji hatua kwa kasi unaoelekea ngazi ya juu zaidi," amesema.
Wakati wa kutekeleza jukumu hilo, wanaanga hao wa Shenzhou-19 waliweka rekodi ya muda mrefu zaidi wa saa 9 wa kufanya kazi moja ya EVA kwa wanaanga wa China.
"Kila EVA yenye mafanikio ni matokeo ya umoja wa wanaanga na juhudi zilizoratibiwa kati ya timu za anga ya juu na za duniani. Pia inaonyesha kikamilifu uhakika wa mavazi yetu ya anga ya juu kwa kazi za nje ya kituo na kujiamini kwa China katika teknolojia ya anga ya juu." amesema Cai.
Wanaanga hao walipanda viazi vitamu kwenye obiti kwa mara ya kwanza na kurekodi hali ya mchakato mzima kuanzia kuota hadi kuvuna.
Pia, walishiriki katika majaribio na upimaji jumla ya 88 wa sayansi na teknolojia ya anga ya juu na miradi ya upimaji wa kisayansi na kutekeleza kazi sita za ubebaji vifaa vya kimsingi ndani na nje ya majukumu ya moduli.
Mwanaanga Wang Haoze aliyetekeleza jukumu la chombo cha kubeba binadamu cha Shenzhou-19 cha China kufanya safari kwenye anga ya juu akionekana kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Julai 9, 2025. (Xinhua/Li Yanchen)
Mwanaanga Cai Xuzhe aliyetekeleza jukumu la chmbo cha kubeba binadamu cha Shenzhou 19 cha China kufanya safari kwenye anga ya juu akionekana kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Julai 9, 2025. (Xinhua/Li Yanchen)
Mwanaanga Song Lingdong aliyetekeleza jukumu la chombo cha kubeba binadamu cha Shenzhou 19 cha China kufanya safari kwenye anga ya juu akionekana kwenye mkutano na waandishi wa habari mjini Beijing, Julai 9, 2025. (Xinhua/Li Yanchen)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma