Idadi ya vifo vinavyotokana na Mpox yafikia 40 huku visa vikizidi 5,400 nchini Uganda

(CRI Online) April 22, 2025

Wizara ya Afya ya Uganda jana Jumatatu ilitangaza kuwa, tangu mlipuko wa ugonjwa wa Mpox utokee nchini humo miezi 9 iliyopita, idadi ya jumla ya visa vya mpox vilivyothibitishwa nchini humo imefikia 5,431, huku vifo 40 vikiripotiwa.

Wizara hiyo imesema kwenye ripoti ya hali ya ugonjwa huo kwamba, jumla ya maambukizi mapya 44 yamerekodiwa katika saa 24 zilizopita, na kwamba hali ya baadhi ya wagonjwa wa Mpox waliolazwa hospitalini inazidi kuwa mbaya.

Ripoti hiyo imesema miji na jamii za wavuvi zinaonyesha viwango vya juu vya maambukizi, huku watu wenye umri wa miaka 25 hadi 29 ndiyo kundi linaloathirika zaidi.

Mwezi uliopita, Shirika la Afya Duniani (WHO) lilionya kuwa Uganda ina idadi kubwa zaidi ya visa vya mpox duniani.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha