

Lugha Nyingine
China yaharakisha ufunguaji mlango wa sekta ya huduma, na kuingiza uhakika zaidi duniani
Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China ikifanya mkutano na waandishi wa habari kuhusu Mpango Kazi Kwa ajili ya Kuharakisha Mradi Jumuishi wa Majaribio ya Kupanua Ufunguaji Mlango wa Sekta ya Huduma mjini Beijing, mji mkuu wa China, Aprili 21, 2025. (Xinhua/Pan Xu)
BEIJING - China inaharakisha ufunguaji mlango wa sekta yake ya huduma kupitia hatua kama vile kuharakisha utekelezaji wa miradi ya majaribio, kupanua mambo husika, na kuongeza majaribio kwa shinikizo la juu na kuiga mifano iliyofanikiwa kwa kuifanya katika maeneo mengine, Wizara ya Biashara ya China imeeleza jana Jumatatu kwenye mkutano na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Habari ya Baraza la Serikali la China.
“Kutokana na kuongezeka kwa hatua za upande mmoja na kujihami kibiashara duniani, msukumo wa China wa kupanua ufunguaji mlango kwa hiari na kwa namna ya utaratibu unawakilisha juhudi zake madhubuti za kuleta uhakika na utulivu zaidi duniani,” amesema Ling Ji, naibu waziri wa biashara ambaye pia ni naibu mwakilishi wa biashara ya kimataifa wa China.
Ling amesema, Baraza la Serikali la China hivi karibuni limeidhinisha mpango unaolenga kupanua mipango jumuishi ya majaribio ili kuharakisha ufunguaji mlango wa sekta ya huduma, ambao unahusisha kazi 155 za majaribio katika maeneo muhimu kama vile ufunguaji mlango wa shughuli muhimu za huduma na kuhimiza uvumbuzi na maendeleo ya kiviwanda.
"Hasa, kazi za majaribio ni pamoja na kuondoa vizuizi vya umiliki wa ubia wa kigeni katika maeneo ya huduma kama vile stoo za programu za simu (app stores) na ufikiaji wa intaneti ndani ya sekta ya mawasiliano," amesema Ling, akiongeza kuwa katika sekta ya afya, kazi za majaribio zinahusisha kuunga mkono madaktari wa kigeni kufungua kliniki nchini China, kuruhusu wataalamu wa matibabu wa kigeni kufanya kazi China kwa muda mfupi, kuhimiza kuanzisha shule za unesi zinazowekezwa kwa mtaji wa kigeni na kuruhusu kuanzisha taasisi zisizo za faida za kutoa huduma za matibabu na kutunza wazee kupitia ufadhili.
Kwa mujibu wa mkutano huo na waandishi wa habari, katika sekta ya mambo ya fedha, kazi za majaribio zinahusisha kuunga mkono maendeleo ya huduma za mambo ya kimataifa na kuvutia kampuni za bima, mifuko ya fedha, mifuko ya pensheni, mashirika ya uidhinishaji na uhakiki, na mifuko ya mazingira, kijamii na usimamizi (ESG) kutoa fedha, uwekezaji na huduma za kiufundi kwa miradi ya kijani.
"Katika sekta ya uuzaji bidhaa, biashara na utalii wa kitamaduni, mashirika ya usafiri wa watalii yanayowekezwa na mtaji wa kigeni yataruhusiwa kutoa huduma za utalii wa nje ya nchi, wakati huohuo sekta ya usafiri itachunguza miundo mipya ya usafiri wa aina mbalimbali, kuunga mkono uuzaji nje magari yanayotumia nishati mpya na betri," Ling amesema.
Tangu mwaka 2015, China imeidhinisha mikoa na miji 11, ikiwemo Beijing na Hainan, kutekeleza mipango ya majaribio, ikiendelea kupanua ufunguaji mlango wa kitaasisi kwa kuzingatia sheria, kanuni, usimamizi na viwango.
Sekta ya huduma ni eneo muhimu kwa uwekezaji wa kigeni nchini China. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, matumizi halisi ya uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) katika sekta ya huduma yalifikia yuan bilioni 193.33 (dola za kimarekani kama bilioni 26.83), ikichukua zaidi ya asilimia 70 ya jumla ya FDI ya nchi, kwa mujibu wa takwimu mpya kutoka Wizara ya Biashara.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma