

Lugha Nyingine
Maelfu ya waandamanaji waandamana kupinga sera za Trump katika sehemu mbalimbali za Marekani
Waandamanaji wakishiriki kwenye maandamano kupinga sera za utawala wa Donald Trump Jijini New York, Marekani, Aprili 19, 2025. (Xinhua/Liu Yanan)
WASHINGTON - Maelfu ya waandamanaji Jumamosi waliandamana barabarani katika miji mbalimbali nchini Marekani katika kile waandamanaji walichoeleza kuwa ni sehemu ya "Siku ya Taifa ya Kuchukua Hatua" dhidi ya sera na kile wanachokiona kuwa matishio ya Rais Donald Trump kwa demokrasia.
Yakiwa yameandaliwa katika siku ya maadhimisho ya kutimia miaka 250 tangu kuanza kwa Vita vya Mapinduzi vya Marekani, maandamano hayo yamehusisha kuanzia matembezi ya maandamano ya makundi katikati ya eneo la Manhattan hadi mikusanyiko ya hadhara nje ya Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., yakileta ufanano wa miito ya kihistoria ya kudai uhuru na madai ya leo ya uwajibikaji wa kiutendaji.
Mjini New York, watu walikusanyika nje ya maktaba kuu ya jiji hilo wakiwa wamebeba mabango yaliyokuwa yakimlenga rais huyo wa Marekani yenye kauli mbiu kama vile "Hakuna Wafalme Marekani” (No Kings in America) na "Pinga Udikteta;" mjini Chicago, waandamanaji wakitamka kaulimbiu ya "Linda demokrasia yetu" walitembea kuupita Ukumbi wa Jiji; mjini San Francisco, washiriki waliunda bango la binadamu lililokuwa likiandika (Mpigie Kura ya Kukosa Imani na Muondoe” (Impeach & Remove) katika Ocean Beach.
Waandamanaji walikuwa wamebeba mabango ya kukemea kufukuzwa nchini kwa haraka wahamiaji, ufukuzaji watu wengi kazini ndani ya wizara za serikali kuu, na kupunguzwa kwa ofisi za Hifadhi ya Jamii, wakati huohuo wengi pia walionyesha kuunga mkono haki za watu waliobadili jinsia na sera kali za tabianchi.
"Tuko katika hali ya hatari ambayo haijapataka kutokea nchini Marekani," amesema Raymond Lotta, mwanauchumi wa kisiasa na mwandishi.
"Trump anafanya mambo yasiyo ya kisheria, na anapaswa kuacha," amesema muandamanaji mwingine aliyejitambulisha kwa jina moja la George. Alikuwa ameshikilia bango lililosomeka "Fukuza Nje ya Nchi Trump" (Deport Trump) kuonyesha hasira yake.
Waandamanaji wakiwa wamekusanyika nje ya Ikulu ya White House mjini Washington, D.C., Marekani, Aprili 19, 2025. (Xinhua/Hu Yousong)
Akiviita vita vya sasa vya kibiashara kuwa "visivyo vya lazima," Chris, muandamanaji mwingine ambaye ametaja jina lake la kwanza tu, amesema, "Kutumia ushuru kunaharibu uchumi wetu. Hasa, kunaathiri uchumi wa dunia. Inasababisha msukosuko mkubwa duniani kote."
"Tayari tunaona dalili za kwanza za mdororo wa uchumi," amesema Chris, ambaye alikuwa ameshikilia bango lililokuwa likisomeka "ushuru sawa na mdororo."
Wakati huo huo, baadhi ya makundi yalijikita katika huduma za jamii, kuandaa mchangowya chakula, kufundisha na kazi ya kujitolea katika makazi ya wenyeji.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wamebainisha kuwa maandamano hayo ya Jumamosi yameonyesha uhamasishaji mkubwa wa pili dhidi ya utawala wa Trump mwezi Aprili, kufuatia wimbi la awali la Aprili 5, na yamedhihirisha mfadhaiko unaoongezeka katika mitaa na kile washiriki wanaona kama mmomonyoko wa mizania na uwajibikaji kati ya mamlaka ya serikali na yale ya mamlaka nyingine za nchi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma