

Lugha Nyingine
Tanzania mbioni kuanzisha usafiri wa vyombo vya kuendeshwa angani kwenye nyaya ili kuchochea utalii
Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu ya Tanzania (LATRA) imesema inajiandaa kuanzisha kanuni za uendeshaji wa usafiri wa vyombo vinavyoendeshwa angani kwenye nyaya (Cable Transport), ili kuimarisha miundombinu ya utalii na usafiri nchini Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa LATRA Bw. Habibu Suluo, amesema mikoa minane ikiwemo ya Dar es Salaam, Arusha, Tanga, Pwani, Morogoro, Mbeya, Kilimanjaro na lringa imetambuliwa kwa ajili ya kuendesha usafiri huo.
Usafiri wa vyombo vya usafiri vya kuendeshwa angani kwenye nyaya ni usafiri wa kusafirisha abiria kwenye vyombo hivyo vinavyoendeshwa angani kwenye nyaya na umeelezwa na mamlaka hiyo kuwa utasaidia watalii kupita kwenye vivutio vya utalii vilivyoko katika maeneo ya milima ndani ya muda mfupi.
Bw. Suluo amesema usafiri huo unaopendekezwa utaanzishwa kwenye Mlima Kilimanjaro, katika maeneo ya milimani kama vile Mbeya na lringa, na katika mikoa yenye msongamano wa watu, ikiwa ni pamoja na Arusha na Dar es Salaam.
Bw. Suluo ameondoa wasiwasi kwamba kuanzishwa kwa usafiri huo kwenye Mlima Kilimanjaro kutasababisha upotezaji ajira kwa wasafirishaji wanaosaidia wapanda mlima, akisema teknolojia hiyo inalenga kutoa chaguo mbadala na siyo kuchukua nafasi za ajira.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma