

Lugha Nyingine
Ukame wazidi kuwa mkali Kenya
Mamlaka ya Taifa ya Kudhibiti Ukame ya Kenya (NDMA) imetahadharisha kuwa hali ya ukame nchini Kenya imezidi kuwa mbaya, huku hali ikizorota katika kaunti zote 23, jambo linalofanya mamilioni ya watu kukabiliwa na hatari ya njaa.
NDMA imesema katika ripoti yake ya hivi karibuni kwamba kaunti 15 ziko katika hali ya "kawaida" ya ukame huku nane zikiwa katika kiwango cha "tahadhari".
Mamlaka hiyo imebaini kuwa kaunti nyingi zinakabiliwa na mvua zinazoweza kufuatiwa na kiangazi na hivyo kuzidisha hali hiyo.
Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imesema misukosuko mingi, inayochochewa na migogoro inayoendelea, ukosefu wa utulivu wa kisiasa, mshtuko wa kiuchumi, milipuko ya magonjwa, na matukio mabaya ya hali ya hewa, vinazidisha mahitaji yaliyopo ya kibinadamu na kuchochea uhamaji wa watu katika Afrika Mashariki.
OCHA imesema hadi kufikia mwezi Machi eneo hilo lina zaidi ya watu milioni 24 waliokimbia makazi yao, wakiwemo wakimbizi na wanaotafuta hifadhi milioni 5.7 na wakimbizi wa ndani milioni 18.8.
Aidha imesema, zaidi ya watu milioni 56 nchini Burundi, Djibouti, Ethiopia, Kenya, Rwanda, Somalia, Sudan Kusini, Sudan, Tanzania, na Uganda wanakabiliwa na msukosuko wa uhaba wa chakula tangu Mei 2024 hadi Juni 2025.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma