

Lugha Nyingine
Biashara ya nje ya China yaongezeka kwa asilimia 1.3 katika robo ya 1, ikiendeleza maendeleo imara
Picha iliyopigwa na droni ikionyesha Bandari ya Tangshan katika Mkoa wa Hebei, kaskazini mwa China, Januari 13, 2025. (Picha na Liu Mancang/Xinhua)
BEIJING – thamani ya jumla ya bidhaa zinazoagizwa na kuuzwa nje ya China imeongezeka kwa asilimia 1.3 mwaka hadi mwaka katika robo ya kwanza ya mwaka huu, ikionyesha ukuaji thabiti na uhimimilivu mkubwa licha ya changamoto za nje, takwimu rasmi kutoka Mamlaka Kuu ya Forodha ya China (GAC) zimeonyesha jana Jumatatu.
Takwimu hizo za GAC zimeonyesha kuwa, mauzo ya nje ya China katika kipindi hicho yalipanda kwa asilimia 6.9 hadi yuan trilioni 6.13 (sawa na dola za kimarekani karibu bilioni 850.1) huku uagizaji bidhaa kutoka nje ukishuka kwa asilimia 6 hadi yuan trilioni 4.17.
"Pamoja na kasi dhaifu ya ukuaji wa uchumi duniani, kuongezeka kwa kujihami kibiashara na mivutano ya siasa za kijiografia, biashara ya nje ya China imedumisha ukuaji thabiti huku kukiwa na maendeleo mapya katika maendeleo yenye sifa bora mwaka huu," Wang Lingjun, naibu mkuu wa GAC, amesema kwenye mkutano na waandishi wa habari.
Kwa mujibu wa takwimu hizo zilizotolewa, biashara ya nje ya nchi hiyo imeendelea kushuhudia uboreshaji wa kimuundo huku uagizaji na uuzaji nje wa sekta ya utengenezaji vifaa ukiongezeka kwa asilimia 7.6 mwaka hadi mwaka katika kipindi cha Januari hadi Machi, ambayo imechukua nusu ya jumla ya biashara ya nje ya nchi hiyo.
Msemaji wa GAC Lyu Daliang amesema kwenye mkutano huo na waandishi wa habari kwamba mauzo ya nje ya China katika nchi na maeneo zaidi ya 170 yaliongezeka katika miezi mitatu ya kwanza, huku ukuaji mkubwa ukishuhudiwa katika sekta za viwanda vya teknolojia za hali ya juu, za kisasa na za kijani.
Mwezi Machi pekee, uagizaji na uuzaji nje bidhaa wa nchi hiyo uliongezeka kwa asilimia 6 kuliko mwaka mmoja uliopita wakati kama huo, kiasi ambacho ni sawa na mwezi Februari na kupungua kwa asilimia 2.2 kuliko mwezi Januari, kwa mujibu wa takwimu hizo za GAC.
Lyu amesema kuwa mauzo ya nje ya China sasa yanakabiliwa na hali ngumu ya nje, lakini "anga haitaanguka."
Wang amesisitiza kwamba "ushuru wa Reciprocal" wa Marekani unapindua utaratibu uliopo wa uchumi na biashara wa kimataifa, kuweka maslahi ya Marekani juu ya manufaa ya pamoja ya jumuiya ya kimataifa, kukiuka kwa kiasi kikubwa sheria za WTO, kudhoofisha mfumo wa biashara wa kimataifa unaozingatia sheria na kuvuruga utaratibu wa uchumi duniani.
"Hakuna mshindi katika vita vya kibiashara, na kujihami kibiashara hakuna njia," amesema.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma