

Lugha Nyingine
Rais wa China akutana na waziri mkuu wa Hispania
(Picha inatoka Xinhua)
Rais Xi Jinping wa China tarehe 11 amekutana na Waziri Mkuu wa Hispania Bw. Pedro Sánchez hapa Beijing.
Kwenye mazungumzo yao, rais Xi amesema, mwaka huu ni kumbukumbu ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa wenzi wa kimkakati wa pande zote kati ya China na Hispania. Amesema China iko tayari kushirikiana na Hispania kujenga uhusiano wao uwe na nguvu za kimkakati na uhai mkubwa wa maendeleo, ili kuleta manufaa kwa watu wa nchi hizi mbili, kukuza zaidi uhusiano kati ya China na Ulaya, na kuchangia zaidi katika kudumisha amani, utulivu, na maendeleo duniani.
Rais Xi ameeleza kuwa, China imekuwa ikiuchukulia Umoja wa Ulaya kama nguzo muhimu ya dunia yenye ncha nyingi, na ni moja ya nchi kubwa zinazounga mkono umoja na maendeleo ya Umoja wa Ulaya. Katika hali ya sasa, China na Umoja wa Ulaya zinapaswa kuimarisha uhusiano wao wa kiwenzi na kushikilia ushirikiano wa kufungua mlango.
Rais Xi amesisitiza kuwa, vita vya ushuru havina mshindi, na kupigana na dunia ni sawa na kujitenga, na kuongeza kuwa, bila kujali jinsi mazingira ya nje yanavyobadilika, China itaendelea kuwa na imani imara, kudumisha mikakati yake na kuendelea na juhudi za kufanya vizuri mambo muhimu ya ndani.
Kwa upande wake, waziri mkuu wa Hispania Bw. Pedro Sánchez amesema kuwa Hispania inathamini uhusiano wake na China, inashikilia imara sera ya “kuwepo kwa China Moja", na iko tayari kushirikiana na China katika ngazi ya juu, kukuza ushirikiano wa kunufaishana katika maeneo ya biashara, uwekezaji, uvumbuzi wa teknolojia, na nishati ya kijani. Pia katika kuongeza mawasiliano katika maeneo ya elimu, utamaduni, na utalii, ili kuleta maendeleo mapya katika uhusiano wa nchi hizi mbili. Ameongeza kuwa China ni mshirika muhimu wa Umoja wa Ulaya, na Hispania daima inaunga mkono maendeleo thabiti ya uhusiano wa Ulaya na China. Umoja wa Ulaya unashikilia biashara huria na wazi, na unajitahidi kulinda utaratibu wa pande nyingi, kupinga vitendo vya kuongeza ushuru kwa upande mmoja. Amesema, vita vya biashara havitakuwa na mshindi. Katika hali ya kimataifa yenye utata, Hispania na Umoja wa Ulaya zinapenda kuimarisha mawasiliano na ushirikiano na China, kulinda utaratibu wa biashara wa kimataifa, kushirikiana katika kukabiliana na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, umasikini, na kulinda maslahi ya pamoja ya jamii ya kimataifa.
Pande hizo mbili pia zimebadilishana maoni kuhusu mgogoro wa Ukraine na masuala mengine.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma