

Lugha Nyingine
Uturuki kuendelea kushirikiana na Indonesia juu ya ukarabati wa Gaza
Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki (kulia, mbele) na Rais Prabowo Subianto wa Indonesia (kushoto, mbele) wakihudhuria mkutano wa pamoja na waandishi wa habari mjini Ankara, Uturuki, tarehe 10 Aprili 2025. (Mustafa Kaya/kupitia Xinhua)
ANKARA - Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuki amesema kwamba nchi yake itaendelea kushirikiana na Indonesia katika ukarabati wa Gaza na kulinda mambo ya Palestina, kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Ikulu ya Uturuki jana Alhamisi.
"Tunathamini msimamo wa Indonesia kuhusu suala la Palestina. Katika kipindi kijacho, tutaendelea kufanya kazi na Indonesia kuijenga upya Gaza na kulinda mambo ya Palestina," Erdogan amesema kwenye mkutano wa pamoja na waandishi wa habari na mwenzake wa Indonesia Prabowo Subianto aliye ziarani nchini humo, kufuatia mkutano kati ya viongozi hao wawili.
Kuhusu uhusiano wa pande mbili, Erdogan amesema pande hizo mbili "zimekubaliana kuanzisha mipango mipya kuhusu ushirikiano wetu katika maeneo yanayogusa kuanzia ulinzi na ujenzi hadi huduma za afya, nishati na chakula."
Amesema pande zote mbili pia zimejadili hatua wezekana za kuongeza biashara ya pande mbili kufikia lengo lao la pamoja la dola za kimarekani bilioni 10 "kwa njia ya uwiano, kwa kuzingatia kunufaishana," akiongeza kuwa wametia saini nyaraka kadhaa kuhusu utamaduni, usimamizi wa maafa na dharura, na mawasiliano.
"Tutaendelea kufanya ushirikiano na Indonesia katika majukwaa yote ya kimataifa," Erdogan amesema.
Ukiacha mkutano huo wa pande mbili, Rais Subianto pia amehutubia Bunge la Uturuki mapema siku hiyo, Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotolewa na Sekretarieti ya Baraza la Mawaziri la Indonesia.
Katika hotuba yake, Rais Subianto amefafanua juu ya "historia ndefu ya mshikamano" kati ya Uturuki na Indonesia, na ameelezea nia ya Indonesia ya kushirikiana na Uturuki kutetea watu wa Palestina dhidi ya mashambulizi ya Israel, na kushughulikia ukiukaji wa haki za binadamu katika Gaza, taarifa hiyo kwa vyombo vya habari imeonyesha.
Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Anadolu linaloendeshwa na serikali ya Uturuki, Rais Prabowo atahudhuria Baraza lijalo la Diplomasia la Antalya lililopangwa kufanyika kuanzia leo Ijumaa hadi Jumapili katika mji wa Antalya nchini Uturuki.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma