EAC yataka kuanzisha utaratibu wa pamoja wa kuzuia mauaji ya kimbari

(CRI Online) April 09, 2025

Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) imehimiza nchi wanachama kuanzisha utaratibu wa pamoja wa kuzuia mauaji ya kimbari na kuchukua hatua stahiki dhidi ya wahalifu kwa mujibu wa itifaki ya umoja huo kuhusu amani na usalama.

Katibu Mkuu wa EAC Veronica Nduva amesema katika taarifa yake Jumatatu kwamba EAC imeanzisha kituo cha tahadhari ya mapema katika makao makuu yake mjini Arusha nchini Tanzania, na vituo vya kitaifa katika nchi kadhaa wanachama, ikiwa na mipango ya kupanua wigo kwa wanachama wote.

Amesema wakati kanda hiyo ikiadhimisha Mauaji ya Kimbari ya 1994 dhidi ya Watutsi nchini Rwanda, ni muhimu kutambua kwamba dalili za tahadhari ya mapema za mauaji ya halaiki, zikiwemo kauli za chuki, uchochezi, ubaguzi wa kikabila, habari potoshi, na kudhalilisha utu, bado zipo hadi leo katika baadhi ya maeneo ya kanda hiyo.

Nduva amefafanua kuwa katika zama ya kidijitali, vitisho hivi vinazidishwa na mitandao ya kijamii na vyombo vingine vya mawasiliano ya watu wengi, vikichangiwa na changamoto kama vile ukosefu wa ajira kwa vijana, mapungufu ya kiutawala na kuenea kwa silaha ndogo ndogo.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha