COMESA na Benki ya Dunia wazindua mpango wa kuwezesha Waafrika milioni 180 kupata mtandao wa intaneti

(CRI Online) April 08, 2025

Soko la Pamoja la Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika (COMESA) na Benki ya Dunia wamezindua mradi unaolenga kuwezesha watu takriban milioni 180 mashariki na kusini mwa Afrika kupata mtandao wa intaneti na kutoa huduma wezeshi za kidijitali kwa watu milioni 100 katika kipindi cha miaka minane ijayo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Jumatatu baada ya uzinduzi wake nchini Zambia, mradi huo wenye thamani ya dola za kimarekani bilioni 2.5, unatarajiwa kunufaisha makundi mbalimbali, yakiwemo ya wanawake, wakimbizi, jamii zinazowahifadhi, kampuni za sekta binafsi na mashirika ya sekta ya umma.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, awamu ya kwanza ya mpango huo inajumuisha ruzuku ya dola za Kimarekani milioni 10 kwa ajili ya sekretarieti ya COMESA na dola za Kimarekani milioni 780 kwa ajili ya shughuli nchini Angola, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Malawi.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha