

Lugha Nyingine
Uzuri wa Majira: Kipindi cha Qingming
Kesho Ijumaa itakuwa Qingming, kipindi cha tano katika vipindi vya hali ya hewa kwa kalenda ya kilimo ya China, na sikukuu ya jadi ya China yenye historia ya maelfu ya miaka.
Katika Hangzhou, mji wenye kupendeza katika mkoa wa Zhejiang, mashariki mwa China, watu hushuhudia mvuto wake wa kipekee katika kipindi hiki.
Wakati wa Qingming, majani hukua kuwa kijani, ndege aina ya orioles huruka angani, matawi ya miti huyumba taratibu kwa upepo, na upepo wa majira ya mchipuko hunong’ona mashairi. Maua huchanua kimyakimya, na watu, kama kwamba kila hatua yao ni sehemu ya shairi, hutembea kwenye Pwani ya Su wakati wa alfajiri wakifurahia mandhari ya kupendeza.
Katika kipindi cha Qingming, Hangzhou hujaa manukato ya mmea wa wormwood. Kila kaya huwa na pilika nyingi kutengeneza au kununua qingtuan, aina ya keki ya kijani mviringo. Kitindamlo hiki laini na kinachonata ni ladha maalum ya msimu wa mchipuko katika maeneo ya kusini mwa Mto Yangtze.
Sikukuu ya Qingming pia ni muda wa kukumbuka wapendwa na kutoa heshima kwa mababu. Nchini China, watu husafisha makaburi na kutoa heshima kwa sadaka kuonyesha majonzi na kumbukumbu.
Nchi nyingine duniani pia zina desturi kama hii. Kwa mfano, watu nchini Mexico, hufanya sherehe za kuenzi maisha na kueleza upendo wa kina kwa wapendwa wao katika Día de los Muertos kila tarehe 1 na 2 Novemba.
Katika kipindi cha Qingming, maua ya pear huyumbayumba kwa upepo, na wasafiri hutoka nje kutafuta majira ya mchipuko. Haijalishi ni namna gani unasherehekea kipindi hiki cha majira, Qingming huleta joto na matumaini.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma