

Lugha Nyingine
Rais Xi na mwenzake wa India watumiana pongezi juu ya maadhimisho ya miaka 75 ya uhusiano
BEIJING - Rais wa China Xi Jinping na mwenzake wa India Droupadi Murmu wametumiana salamu za kupongeza maadhimisho ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.
Katika salamu yake ya pongezi iliyotumwa Jumanne, Rais Xi amesema China na India zikiwa nchi za ustaarabu wa kale, nchi kubwa zinazoendelea na nchi muhimu za " Kusini ya Dunia," zote ziko katika hatua muhimu ya juhudi zao za ujenzi wa mambo ya kisasa.
"Maendeleo ya uhusiano kati ya China na India yanaonyesha kwamba ni chaguo sahihi kwa China na India kuwa washirika wa kufanikishana na kufikia 'Tango la Dragoni-Tembo,' ambalo linalingana kikamilifu maslahi ya msingi ya nchi zote mbili na watu wao,” Rais Xi amesema.
Ametoa wito kwa pande zote mbili kutendea na kushughulikia uhusiano wa pande mbili kutoka ngazi ya kimkakati na mtazamo wa muda mrefu, kutafuta njia ya kuishi pamoja kwa amani, kuaminiana, kunufaishana na kupata maendeleo kwa pamoja, kutendana kwa ujirani mwema na kufanya juhudi kwa pamoja kuhimiza Dunia ya ncha nyingi na demokrasia zaidi katika uhusiano wa kimataifa.
Rais Xi pia amesema anapenda kufanya juhudi pamoja na Rais Murmu kuchukua maadhimisho hayo ya uhusiano kama fursa ya kuongeza kuaminiana kimkakati, kuimarisha mawasiliano na ushirikiano katika sekta mbalimbali, kuongeza mawasiliano na uratibu katika mambo makubwa ya kimataifa, kwa pamoja kulinda amani na utulivu katika eneo la mpaka wa China na India, kusukuma mbele maendeleo mazuri na tulivu ya uhusiano wa pande mbili na kutoa mchango kwa ajili ya kuhimiza amani na ustawi wa dunia.
Kwa upande wake, Rais Murmu amesema India na China ni nchi mbili kubwa jirani ambazo idadi ya jumla ya watu wao inachukua theluthi moja ya idadi ya watu wote duniani, na uhusiano tulivu unaotazamiwa na wa kirafiki kati ya pande mbili utazinufaisha nchi hizo mbili na dunia.
Amependekeza kuchukua maadhimisho hayo ya miaka 75 tangu kuanzishwa kwa uhusiano wa kidiplomasia kuwa fursa ya kuhimiza kwa pamoja maendeleo mazuri na tulivu ya uhusiano kati ya India na China.
Siku hiyo, Waziri Mkuu wa China Li Qiang na Waziri Mkuu wa India Narendra Modi pia walitumiana salamu za pongezi.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma