Rais wa Iran akataa mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 31, 2025

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Septemba 16, 2024. (Xinhua/Shadati)

Rais wa Iran Masoud Pezeshkian akihudhuria mkutano na waandishi wa habari mjini Tehran, Iran, Septemba 16, 2024. (Xinhua/Shadati)

TEHRAN - Rais wa Iran Masoud Pezeshkian amethibitisha jana Jumapili kwamba Tehran imekataa kufanya mazungumzo ya moja kwa moja na Marekani akijibu barua kutoka kwa Rais Donald Trump wa Marekani. Hata hivyo, amesisitiza kuwa Iran haijafunga mlango wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, njia ambayo imekuwa ikiiweka wazi mara kwa mara.

Pezeshkian ametoa kauli hiyo kwenye kikao cha baraza la mawaziri mjini Tehran akitoa jibu rasmi la Iran kwa barua hiyo ya Trump iliyotaka mazungumzo ya moja kwa moja kuhusu mpango wa nyuklia wa Tehran.

Barua hiyo iliyotumwa mapema mwezi huu, iliwasilishwa kupitia Umoja wa Falme za Kiarabu, huku jibu la Iran likiwasilishwa Marekani kupitia Oman.

Kwa mujibu wa Pezeshkian, wakati Iran imekataa uwezekano wa mazungumzo ya moja kwa moja, imesisitiza uwazi wake kwa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja, msimamo ambao imekuwa ikiudumisha kwa miaka mingi.

"Hatujawahi kamwe kufunga mlango wa mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja," amesema, akiongeza kuwa kushindwa kupata maendeleo katika mazungumzo ya zamani kumetokana na ahadi zisizotekelezwa na Marekani, ambazo, amependekeza, lazima zishughulikiwe ili kujenga upya hali ya kuaminiana.

"Tabia ya Marekani itaamua mwendelezo wa njia ya mazungumzo," amesema, akiashiria kwamba mtazamo wa Iran unabakia kutegemea hatua za Marekani.

Mapema mwezi Machi, Trump alisema kuwa alikuwa ametuma barua kwa viongozi wa Iran, akipendekeza mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Seyed Abbas Araghchi alithibitisha Alhamisi wiki iliyopita kwamba Iran imetuma jibu lake rasmi kupitia Oman siku iliyopita (yaani Jumatano wiki iliyopita), ikisisitiza kukataa kwake kufanya mazungumzo ya moja kwa moja, haswa chini ya kampeni inayoendelea ya "shinikizo la juu" na vitisho vya kijeshi kutoka kwa Marekani.

Makubaliano hayo ya nyuklia ambayo yanajulikana kwa jina rasmi la Mpango Jumuishi wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) yalitiwa saini mwaka 2015 kati ya Iran na nchi zenye nguvu duniani. Chini ya makubaliano hayo, Iran ilikubali kupunguza mpango wake wa nyuklia kwa sharti la kuondolewa vikwazo. Hata hivyo, Mei 2018, wakati wa muhula wa kwanza wa Trump, Marekani ilijitoa kwenye makubaliano hayo na kuweka vikwazo tena, ikiifanya Iran kupunguza ahadi zake za nyuklia.

Juhudi za kufufua makubaliano hayo ya nyuklia hadi sasa zimepiga hatua ndogo, huku jitihada za kidiplomasia zikikwama na mvutano kati ya Iran na Marekai ukiendelea kuwa juu.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha