

Lugha Nyingine
China yaitaka Marekani kutoelekeza mantiki yake ya umwamba kwa China
BEIJING - China inaitaka Marekani kutoelekeza mantiki yake ya umwamba kwa China au kuutazama uhusiano kati ya China na Marekani kupitia mawazo ya Vita Baridi yanayopitwa na wakati, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya China Guo Jiakun amesema.
Guo ametoa kauli hiyo jana Jumatano kwenye mkutano na waandishi wa habari wakati akijibu swali la vyombo vya habari kuhusu ripoti ya Marekani iliyodai kuwa China ni nchi ya kwanza inayoleta tishio kwa Marekani kijeshi na katika mtandao.
Amesema, Marekani inatoa ripoti hizo zisizowajibika na zenye upendeleo mwaka baada ya mwaka, ikieneza "tishio la China" na kuchochea ushindani wa hali ya juu kati ya nchi kubwa, kama kisingizio tu cha kuizuia na kuikandamiza China, na kudumisha umwamba wake yenyewe.
"Maendeleo ya China yanatokana na mantiki ya wazi ya kihistoria na nguvu kubwa ya ndani. Malengo yetu ya wazi yanayotafutwa, ni kuwafanya tu watu wa China waishi maisha bora na kutoa mchango mkubwa zaidi kwa dunia. Hatuna nia ya kuipita au kuchukua nafasi ya nchi yoyote," Guo amesema.
Amesema suala la Taiwan ni mambo ya ndani kabisa ya China, akiongeza kuwa China bado inashikilia azma yake ya kupinga "kujitenga kwa Taiwan" na kulinda mamlaka na ukamilifu wa ardhi ya taifa, na kwamba hakuna yeyote anayepaswa kudharau au kulifanyia maamuzi potofu hili.
"Tunaitaka Marekani isielekeza mantiki yake ya umwamba kwa China au kutazama uhusiano kati ya China na Marekani kupitia mtazamo wa Vita Baridi unaopitwa na wakati, na siyo kuizuia na kuikandamiza China kwa kisingizio cha ushindani wa kimkakati," Guo amesema.
Ameongeza kuwa Marekani inapaswa kuacha kula njama na kuunga mkono vikundi vya kutafuta "kujitenga kwa Taiwan" kwa namna yoyote ile, na kuacha kueneza "tishio la China". Badala yake, inapaswa kuchukua hatua madhubuti ili kuhimiza maendeleo tulivu, yenye afya na endelevu ya uhusiano kati ya China na Marekani.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma