

Lugha Nyingine
Maofisa Watendaji Wakuu wa kampuni za kimataifa waenda China kwa fursa za biashara
Picha hii iliyopigwa Machi 23, 2025 ikionesha Kongamano juu ya Sera za Jumla na Ukuaji Uchumi la Jukwaa la Ngazi ya Juu la Maendeleo la China (CDF) Mwaka 2025 mjini Beijing. (Xinhua/Li Xin)
Viongozi wa kampuni kubwa za kimataifa takriban 80, zikiwemo Siemens, Apple, Samsung, na Pfizer, wamekwenda China kutafuta fursa mpya za ushirikiano na nchi hiyo yenye uchumi wa pili kwa ukubwa duniani.
Wakuu hao walihudhuria Jukwaa la Maendeleo la China 2025, lililofanyika Beijing kuanzia Machi 23 hadi 24. Tukio hilo la kila mwaka, lililoandaliwa na Kituo cha Utafiti wa Maendeleo cha Baraza la Serikali la China, limekuwa jukwaa muhimu la mazungumzo kwa serikali ya China, kampuni za kimataifa, wasomi, na mashirika ya kimataifa.
Waziri Mkuu wa China, Li Qiang, katika hotuba yake ya ufunguzi wa jukwaa hilo, alisema kuwa China itaendelea kukaribisha kampuni kutoka duniani kote kwa mikono miwili, kupanua zaidi ufikiaji wa soko, kushughulikia ipasavyo masuala ya kampuni, na kuwezesha ujumuishaji wa kina zaidi wa kampuni zinazowekezwa kwa mtaji wa nje katika soko la China.
Kabla ya jukwaa hilo, kampuni kubwa ya dawa ya Uingereza, AstraZeneca, ilitia saini makubaliano ya aina yake ya uwekezaji wenye thamani ya dola bilioni 2.5 za Marekani siku ya Ijumaa, ili kuwekeza mjini Beijing katika kipindi cha miaka mitano ijayo, ikiwa ni uwekezaji mkubwa zaidi wa mara moja katika sekta ya dawa za binadamu jijini Beijing katika miaka ya hivi karibuni.
Chini ya makubaliano hayo, AstraZeneca itaanzisha kituo cha kimataifa cha kimkakati cha Utafiti na Maendeleo (R&D) jijini Beijing, ambacho kitakuwa cha sita duniani na cha pili nchini China baada ya kile cha Shanghai. Kituo hicho kipya, kikiwa na maabara ya hali ya juu ya AI na sayansi ya data, kitaharakisha utafiti wa awali wa dawa na maendeleo ya majaribio ya matibabu.
"Uwekezaji huu unaonyesha imani yetu kwa mfumo wa uvumbuzi wa sayansi ya maisha wa Beijing wenye kiwango cha dunia, fursa nyingi za kiushirikiano, na hazina kubwa ya vipaji," alisema Pascal Soriot, Ofisa Mtendaji Mkuu wa AstraZeneca, katika mahojiano na Shirika la Habari la China, Xinhua.
Mwaka 2024, BMW iliwasilisha kwa wateja wa China zaidi ya magari 100,000 ya betri kwa mara ya kwanza, ikiifanya China kuwa soko lake kubwa zaidi la magari yanayotumia umeme duniani.
Kwenye mkutano na Waziri wa Biashara wa China Wang Wentao, mwenyekiti wa bodi ya wasimamizi wa BMW Oliver Zipse alisema kuwa kampuni hiyo ina dhamira ya kupanua uwekezaji wake nchini China na kuharakisha ujanibishaji wa uzalishaji vilevile utafiti na maendeleo.
Takwimu kutoka mamlaka husika zimeonyesha kuwa China inaendelea kuwa kivutio kikuu cha uwekezaji wa kimataifa. Kampuni karibu 60,000 zinazowekezwa na mtaji wa kigeni zilianzishwa China Mwaka 2024 pekee, ongezeko la asilimia 9.9 ikilinganishwa na mwaka uliopita.
Kiwango cha kurejea uwekezaji wa moja kwa moja wa kigeni (FDI) nchini China kimebaki takriban asilimia 9 katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, kikiwa miongoni mwa viwango vya juu zaidi duniani.
Ripoti ya kazi ya serikali ya mwaka huu inasisitiza kuwa China itaendelea kuhamasisha wawekezaji wa kigeni kuongeza uwekezaji wao nchini humo, na itahakikisha utendeaji kwa usawa wa kampuni zinazowekezwa kwa mtaji wa kigeni katika nyanja kama vile upatikanaji wa rasilimali za uzalishaji, maombi ya leseni, uwekaji wa viwango, na manunuzi ya serikali.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma