Balozi wa Afrika Kusini aliyefukuzwa nchini Marekani arejea nyumbani bila "majuto"

(CRI Online) Machi 24, 2025

Balozi wa Afrika Kusini aliyefukuzwa nchini Marekani Ebrahim Rasool amesema Jumapili kwamba amerejea nyumbani bila "majuto."

Rasool na mkewe, Rosieda, waliwasili katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Cape Town Jumapili asubuhi na kupata makaribisho makubwa kutoka kwa mamia ya wafuasi.

Mapema mwezi huu, Rasool alitangazwa kuwa "mtu asiyekaribishwa" na Marekani, kufuatia kauli za awali alizotoa kwenye mkutano ulioandaliwa na Taasisi ya Mapungubwe ya Tafakari ya Kimkakati, ambayo ni jopo la washauri bingwa nchini Afrika Kusini, ambapo alimkosoa Rais wa Marekani Donald Trump.

Akiwahutubia wafuasi wapatao 300 kwenye uwanja huo wa ndege, Rasool amesema kwamba ingawa alitangazwa kuwa mtu asiyekaribishwa Marekani kwa minajili ya kumdhalilisha, mapokezi hayo mazuri yamegeuza hadhi hiyo kuwa ya heshima.

Rasool anatarajia kuwa Rais Cyril Ramaphosa atampata mtu mwenye uwezo wa kurekebisha uhusiano na Marekani bila kuachana na maadili ya Afrika Kusini, akisisitiza kwamba lazima wapiganie hilo, na ni lazima wadumishe heshima yao.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha