Wang Yi akutana na makundi ya urafiki kati ya Japan na China

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 24, 2025
Wang Yi akutana na makundi ya urafiki kati ya Japan na China
Wang Yi, mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) ambaye pia ni mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya CPC, akikutana na wawakilishi kutoka makundi saba ya urafiki kati ya Japan na China mjini Tokyo, Japan, Machi 23, 2025. (Xinhua/Jia Haocheng)

TOKYO - Wang Yi, Mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China ambaye pia ni Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya CPC, amekutana na wawakilishi kutoka makundi saba ya urafiki kati ya Japan na China, akielezea umuhimu wa ushirikiano wa pande mbili chini ya hali ya kutokuwa na uhakika duniani.

Akibainisha kuongezeka kukosekana utulivu katika hali ya kimataifa, Wang amesisitiza kuwa, China imeazimia kubeba majukumu yake kama nchi kubwa, kushirikiana na nchi nyingine kulinda amani na usalama barani Asia, na kuhimiza maendeleo ya binadamu.

Wang amesema, China na Japan zikiwa nchi majirani wa karibu na zenye uchumi mkubwa duniani, lazima zitathmini upya thamani ya uhusiano wao, kusisitiza umuhimu wa urafiki wao, kuimarisha ushirikiano wa kunufaishana, kuongeza nguvu ya uhusiano wa kirafiki kati ya watu na watu ili kuhimiza maendeleo endelevu, mazuri na imara ya uhusiano kati ya China na Japan.

Huku akitambua kujitolea kwa muda mrefu kwa makundi hayo saba ya urafiki katika kuendeleza urafiki kati ya nchi hizo mbili, Wang ameyahimiza kusonga mbele katika mwelekeo wa ushirikiano wa amani na kirafiki ili kutoa mchango mpya katika kulinda maslahi ya kimsingi ya watu wa nchi zote mbili.

Ametaja maeneo matatu muhimu ya kuimarisha uhusiano, yakijumuisha kudumisha msingi wa kisiasa, kuongeza mazungumzo na mawasiliano katika sekta mbalimbali, na kuandaa warithi wa urafiki kati ya China na Japan.

Pia ametoa wito wa kuhimiza kizazi cha vijana kushiriki kikamilifu katika juhudi za urafiki, kuhakikisha urithi wa ushirikiano wa pande mbili unaendelezwa.

Waliohudhuria mkutano huo ni Hiroshi Moriyama, mwenyekiti wa Umoja wa Wabunge wa Urafiki kati ya Japan na China ambaye pia ni katibu mkuu wa chama tawala cha Japan cha Liberal Democratic, Rais wa Jumuiya ya Japan kwa ajili ya Kuhimiza Biashara ya Kimataifa Yohei Kono, vilevile viongozi wa makundi mengine ya kirafiki.

Wawakilishi wa makundi hayo wamesisitiza umuhimu wa urafiki kati ya China na Japan kwa nchi yao na watu wake, wakiahidi kuendelea kuhimiza mawasiliano katika ngazi ya serikali za mitaa na vijana na kuimarisha zaidi uhusiano kati ya watu wa China na Japan.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha