UN yasema usafirishaji wa misaada kwa kambi ya wakimbizi ya Zamzam inayokumbwa na njaa umekatizwa

(CRI Online) Machi 21, 2025

Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema waasi wenye silaha wameitenga kambi kubwa ya wakimbizi ya Zamzam inayokumbwa na baa la njaa nchini Sudan kwa kukata utoaji wa maji na kuzuia usafirishaji wa misaada.

Ofisi ya Umoja wa Mataifa Inayoratibu Masuala ya Kibinadamu (OCHA) imeonya kuwa hali ya afya katika kambi hiyo iliyoko umbali wa kilomita 12 kusini mwa El Fasher, mji mkuu wa Jimbo la Darfur Kaskazini, inazorota.

Kwa mujibu wa OCHA, makundi yenye silaha yanayosonga mbele kuelekea El-Fasher na Zamzam yametwaa udhibiti kamili wa njia za usafiri, ambapo usafiri wa barabara kati ya El Fasher na Zamzam umekatika kabisa, na hivyo kukwamisha operesheni za kusafirisha misaada na wagonjwa.

Licha ya hali hiyo, wakimbizi wanaendelea kutafuta hifadhi katika kambi ya Zamzam, ambayo kwa sasa imekuwa na watu wapatao laki tano.

(Wahariri wa tovuti:Song Ge,Zhao Jian)

Picha