

Lugha Nyingine
China yapenda kulinda kwa pamoja mfumo wa kweli wa pande nyingi na Ufaransa, asema Wang Yi
BEIJING – Wang Yi, Mkurugenzi wa Ofisi ya Kamati ya Mambo ya Nje ya Kamati Kuu ya Chama cha Kikomunisti cha China (CPC) amesema kwamba China inapenda kudumisha mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu na Ufaransa, kuimarisha uratibu wa kimkakati, na kulinda kwa pamoja mfumo wa kweli wa pande nyingi.
Wang, ambaye pia ni mjumbe wa Ofisi ya Siasa ya Kamati Kuu ya CPC, ametoa kauli hiyo Jumanne alipofanya mazungumzo kwa njia ya simu na Emmanuel Bonne, mshauri wa kidiplomasia wa Rais wa Ufaransa.
Katika mazungumzo hayo kwa njia ya simu, Wang amemwomba Bonne kufikisha salamu za Rais Xi Jinping wa China kwa Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron.
"Hali ya sasa ya kimataifa inazidi kuwa tata na yenye mabadiliko mara kwa mara, huku kukiwa na kuongezeka kwa hali ya kutokuwa na uhakika na kukosekana kwa utulivu," amesema Wang.
Huku akibainisha kuwa mwaka huu ni maadhimisho ya miaka 80 tangu ushindi wa Vita vya Pili vya Dunia, Wang amesema ni muhimu kwa China na Ufaransa, kama nchi wajumbe wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na washirika wa kimkakati wa pande zote, kuimarisha mawasiliano ya kimkakati katika wakati huu muhimu wa kihistoria.
Wang amesema, China inapenda kudumisha mawasiliano ya karibu ya ngazi ya juu na Ufaransa, kuimarisha uratibu wa kimkakati, kulinda kwa pamoja mfumo wa kweli wa pande nyingi, kushikilia hadhi ya Umoja wa Mataifa, kulinda utaratibu wa biashara ya kimataifa, kuhakikisha utulivu wa minyororo ya viwanda na usambazaji duniani, kupinga umwamba wa upande mmoja, kukataa kuweka maslahi ya nchi moja juu ya maslahi ya pamoja ya nchi mbalimbali, ili kuzuia dunia isirudi kwenye sheria za mwituni.
“Katika hali ya sasa, kuna umuhimu mkubwa kwa China na Ulaya kutatua mikwaruzano mahsusi ya kiuchumi na kibiashara kupitia mashauriano,” amesisitiza Wang Yi, akibainisha kuwa China inatumai kuwa Ufaransa itashirikiana na China kutuma ishara chanya ya mshikamano na ushirikiano na kuhimiza maendeleo mazuri na tulivu ya uhusiano kati ya China na Ufaransa na China na Ulaya.
Kwa upande wake Bonne amemwomba Wang kufikisha salamu za Rais Macron kwa Rais Xi. Amesema Ufaransa inaweka umuhimu mkubwa na kuthamini urafiki na hali ya kuaminiana kati ya Ufaransa na China na kwamba chini ya hali tata ya sasa ya kimataifa hasa, Ufaransa inatazamia kudumisha mawasiliano ya ngazi ya juu na mawasiliano ya karibu ya kimkakati kati yake na China ili kupinga kwa pamoja mapambano ya kambi.
Bonne amesema kuwa Ufaransa inapinga vita vya kibiashara na vita vya ushuru, na inapenda kutatua ipasavyo mikwaruzano ya kiuchumi na kibiashara kupitia mazungumzo na China.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma