

Lugha Nyingine
Kituo cha redio na televisheni kilichojengwa kwa msaada wa China chakabidhiwa kwa Shelisheli
Balozi wa China katika nchi ya Visiwa vya Shelisheli Lin Nan akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi mradi wa Kituo cha Radio na Televisheni cha Shelisheli kilichojengwa kwa msaada wa China huko Victoria, mji mkuu wa Shelisheli, Machi 18, 2025. (Xinhua/Dong Jianghui)
VICTORIA - Mradi wa Kituo cha Redio na Televisheni cha Shelisheli uliojengwa kwa msaada wa China umekabidhiwa rasmi kwa nchi hiyo ya Visiwa vya Shelisheli kwenye hafla iliyofanyika jana Jumanne huko Victoria, mji mkuu wa nchi hiyo ya kisiwa cha Bahari ya Hindi.
Ukiwa umejengwa na kampuni Na. 6 ya Uhandisi ya Hunan, mradi huo ulianzishwa mwaka 2018, ukijengwa kwenye eneo lenye ukubwa wa takriban mita za mraba 5,600. Katika majengo ya kituo hicho kuna nyumba za teknolojia ya hali ya juu za redio na televisheni, nafasi za ofisi na vifaa vya kisasa vya mfumo wa utangazaji.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Balozi wa China nchini Shelisheli Lin Nan amesema uhusiano kati ya China na Shelisheli ni mfano wa udhati na urafiki, wa kutendeana kwa usawa, kuungana mkono, na kufanya ushirikiano wa manufaa kwa pande zote kati ya nchi kubwa na ndogo.
Amesema kuwa Mkutano wa Kilele wa Baraza la Ushirikiano kati ya China na Afrika mwaka 2024 uliofanyika Beijing ulishuhudia viongozi wakuu wa nchi hizo mbili kwa pamoja wakiinua hadhi ya uhusiano wa pande mbili kuwa uhusiano wa wenzi wa ushirikiano wa kimkakati, wakiainisha dira ya ushirikiano wa siku za baadaye.
Lin amesisitiza kazi muhimu ya utangazaji katika jamii ya kisasa, si kama tu ni njia kuu ya uenezaji habari, bali pia ni msukumo kwa uhifadhi wa utamaduni, huduma za kijamii, na maendeleo ya nchi.
Amesema makabidhiano hayo rasmi ya mradi huo yanaonesha hatua mpya katika mawasiliano ya kitamaduni na ushirikiano kati ya China na Shelisheli.
Kwa upande wake Makamu Rais wa Shelisheli Ahmed Afif ameishukuru China kwa mradi huo, akiuelezea kuwa ni ushuhuda wa urafiki mkubwa kati ya nchi hizo mbili. "Asante sana China kwa zawadi hii. Ni nguvu halisi ya uhusiano kati ya Shelisheli na China," amesema.
Afif pia ameeleza imani kuwa kituo hicho kitastawisha shughuli za vyombo vya habari vya Ushelisheli, kikihimiza ukuaji na hatimaye kufaidisha nchi nzima. "Seychelles inatarajia ushirikiano huu mzuri kati ya Shelisheli na China," ameongeza.
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma