

Lugha Nyingine
Wataalamu wa China waanza mafunzo ya siku 14 kuhusu mkaa wa mianzi nchini Uganda
Washiriki wakitembelea maonyesho ya bidhaa za mianzi za China kwenye hafla ya ufunguzi wa Kozi ya Mafunzo nchini Uganda juu ya Uchakataji Mkaa kupitia Matumizi ya Mbao na Mianzi mjini Kampala, Uganda, Machi 16, 2025. (Picha na Ronald Ssekandi/Xinhua)
KAMPALA - Timu ya wataalam wa China walioko ziarani imeanza kozi ya mafunzo ya siku 14 kwa wakulima na wadau wa sekta hiyo nchini Uganda kuhusu uzalishaji na matumizi ya mkaa wa mianzi ambapo Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong, ambaye amezindua mafunzo hayo katika mji mkuu wa Uganda, Kampala, amesema elimu na maendeleo ya kijani ni sehemu muhimu za ushirikiano kati ya nchi hizo mbili.
Kwa vile tasnia ya mianzi imekuwa moja ya tasnia muhimu za kijani zinazohakikisha maendeleo endelevu, Zhang ameelezea matumaini kwamba wakati wa kozi hiyo ya mafunzo, washiriki watajifunza na kubadilishana maoni juu ya matumizi ya mianzi katika teknolojia ya uchakataji mkaa.
"Utamaduni wa mianzi una nafasi muhimu nchini China, ukiashiria uhimilivu, unyenyekevu, na maadili ya hali ya juu. Natumai hizi pia zitakuwa sifa za uhusiano wetu, ikijumuisha uhimilivu, kuheshimiana, kujitegemea, na kushikilia kanuni," Zhang amesema.
Wu Tonggui, makamu mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Taifa cha Utafiti wa Mianzi cha China (CNBRC), ambaye ameongoza timu hiyo ya wataalam, amesema mianzi inatambulika sana kama rasilimali mbadala, rafiki kwa mazingira huku ikiwa na faida kubwa za kijamii, kiuchumi na kiikolojia.
Kwa upande wake Margaret Adata, kaimu kamishna wa Idara ya Uungaji Mkono wa Sekta ya Misitu chini ya Wizara ya Maji na Mazingira ya Uganda, amesema muundo wa nishati wa Uganda unabakia kutegemea zaidi mimea asilia.
Adata amesema takwimu za mwaka 2021 zinaonyesha kuwa nishati ya viumbe (hasa kuni na mkaa) inachukua asilimia 87 ya matumizi ya mwisho ya nishati kitaifa, huku mkaa ukiwa ni nishati kuu ya kupikia katika maeneo ya mijini. Amesema, utegemezi huu wa kupita kiasi umesababisha masuala makubwa ya uharibifu wa misitu.
Florence Munaba, katibu mkuu wa Jumuiya ya Mianzi ya Uganda (UBA), kikundi kinachowakilisha wazalishaji mianzi, ameyaelezea mafunzo hayo kama mwanzo wa ukurasa mpya wa kuongeza thamani na matumizi endelevu ya rasilimali za mianzi kwa matumizi ya nishati.
Kwa mujibu wa Wizara ya Maji na Mazingira ya Uganda, serikali imeanzisha mkakati wa kitaifa wa mianzi unaolenga kulima mianzi kwenye ardhi binafsi yenye ukubwa wa hekta 300,000 ifikapo mwaka 2029. Hii inakamilishwa kuanzisha mnyororo wa viwanda vya uchakataji mianzi ambao unahusisha sekta nyingi, kuanzia utengenezaji wa samani hadi uzalishaji wa nishati ya viumbe.
Hafla ya ufunguzi wa Mafunzo nchini Uganda juu ya Uchakataji Mkaa kupitia Matumizi ya Mbao na Mianzi mjini Kampala, Uganda, Machi 16, 2025. (Picha na Ronald Ssekandi/Xinhua)
Wu Tonggui (kushoto), naibu mkurugenzi mkuu wa Kituo cha Tifa cha Utafiti wa Mianzi cha China (CNBRC) akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Mafunzo nchini Uganda juu ya Uchakataji Mkaa kupitia Matumizi ya Mbao na Mianzi mjini Kampala, Uganda, Machi 16, 2025. (Picha na Ronald Ssekandi/Xinhua)
Balozi wa China nchini Uganda Zhang Lizhong (katikati) akizungumza kwenye hafla ya ufunguzi wa Kozi ya Mafunzo nchini Uganda juu ya Uchakataji Mkaa kupitia Matumizi ya Mbao na Mianzi mjini Kampala, Uganda, Machi 16, 2025. (Picha na Ronald Ssekandi/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma