

Lugha Nyingine
Watu 59 wafariki na wengine zaidi ya 100 kujeruhiwa katika ajali ya moto kwenye klabu ya usiku nchini Macedonia Kaskazini
Picha hii iliyopigwa Machi 16, 2025 ikionyesha mahali pa ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
SKOPJE – Watu takriban 59 wamefariki dunia, na wengine zaidi ya 100 kulazwa hospitalini baada ya moto mkali kuzuka jana Jumapili kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, vyombo vya habari nchini humo vimeripoti.
Mamlaka zinasema kuwa moto huo umesababishwa na madoido ya cheche za moto ambazo zimelipua vitu vya dari ya ukumbi huo vinavyoweza kuwaka, ikisababisha moto na moshi mkubwa kuenea kwa kasi. Picha za video zinazosambaa mtandaoni zinaonyesha dari ikiwa inateketea kwa moto huku watu wakihangaika kutoroka.
Waziri wa Mambo ya Ndani wa nchi hiyo Panche Toshkovski amethibitisha kuwa 18 kati ya waliojeruhiwa wako katika hali mbaya.
Miongoni mwa waliolazwa hospitalini ni Vladimir Blazevski, msanii wa kundi la muziki wa hip-hop la DNK, ambaye amepata majeraha ya moto lakini bado yuko katika hali nzuri.
Polisi wanamshikilia mshukiwa mmoja na kutoa hati ya kumkamata wengine wanne akiwemo mmiliki wa klabu hiyo. Wachunguzi wa tukio hilo wanajikita katika uwezekano wa ukiukaji na uzembe wa kiusalama.
Serikali ya Macedonia Kaskazini imeahidi kufanya uchunguzi wa kina ili kuzuia ajali kama hiyo katika siku zijazo. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Hristijan Mickoski amefuta ziara yake iliyopangwa kwenda Montenegro na kusafiri hadi Kocani, eneo la ajali hiyo, ili kusimamia juhudi za uokoaji.
Naye Waziri wa Sheria wa nchi hiyo Igor Filkov ametoa wito wa uwajibikaji, akisisitiza kuwa janga kama hilo halipaswi kutokea tena.
Kamishna wa Upanuzi wa Umoja wa Ulaya, Marta Kos pia ametoa salamu za rambirambi kwa waathiriwa na familia zao.
Polisi wakionekana karibu na mahali pa ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
Watu wakionekana karibu na mahali pa ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
Polisi wakiwa katika ulinzi karibu na mahali pa ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
Watu wakiwa wamekusanyika hospitalini baada ya ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
Watu wakiwa wamekusanyika hospitalini baada ya ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
Ambulensi za jeshi zikiendeshwa kuelekea hospitalini baada ya ajali ya moto kwenye klabu ya usiku mjini Kocani, Macedonia Kaskazini, Machi 16, 2025. (Picha na Tomislav Georgiev/Xinhua)
people.cn © Tovuti ya Gazeti la Umma