Mwanamfalme wa Saudi Arabia akutana na Marco Rubio kabla ya mazungumzo kati ya Marekani na Ukraine

(Tovuti ya Gazeti la Umma) Machi 11, 2025

JEDDAH, Saudi Arabia - Mwanamfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman Al Saud amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani Marco Rubio mjini Jeddah, Saudi Arabia, jana Jumatatu, Kituo cha Televisheni cha Serikali ya Saudi Arabia, Al-Arabiya kimeripoti. Rubio aliwasili katika mji huo wa pwani mapema siku hiyo ya Jumatatu, kwa mkutano kati ya wajumbe wa Marekani na Ukraine.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani ilisema katika taarifa yake ya mapema Jumapili kwamba Rubio atakuwa katika mji huo wa Jeddah kuanzia Jumatatu hadi Jumatano, ambapo atakutana na ujumbe wa Ukraine "ili kusongesha mbele lengo la Rais (Trump) la kumaliza vita vya Russia-Ukraine."

Kwa mujibu wa kituo hicho cha televisheni cha Al-Arabiya, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kwenye ndege kuelekea Jeddah, Rubio alieleza matumaini yake kuhusu mkutano huo ujao na ujumbe wa Ukraine, ingawa aliongeza kuwa kulikuwa bado na mambo zaidi ya kufanyiwa kazi kuhusu mkataba wa madini kati ya Marekani na Ukraine.

Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky pia amewasili Jeddah siku hiyo ya Jumatatu na anatarajiwa kukutana na mwana mfalme huyo wa Saudi Arabia.

(Wahariri wa tovuti:Zhou Linjia,Zhao Jian)

Picha